Pichani ni Moja ya trekta lililokabidhiwa na Wizara ya Kilimo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Februari 22, 2025.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akishuhudia Makabidhiano ya trekta 5 kati ya Wizara ya Kilimo na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Februari 22, 2025.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Wakulima baada ya Makabidhiano ya trekta 5 kati ya Wizara ya Kilimo na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Februari 22, 2025.
Na. Mwandishi Wetu, Ruangwa.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Februari 22, 2025 ameshuhudia makabidhiano ya trekta tano kati ya Wizara ya Kilimo na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango wa Serikali wa kukabidhi zana za kilimo kwenye vituo 45 vya zana nchini.
Akizungumza wakati wa Makabidhiano hayo Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi watakaopata fursa ya kutumia matrekta hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu, kuleta tija na kutimiza malengo yaliyokusudiwa
"Tunauzoefu wa matrekta tuliyoyaleta kipindi cha nyuma, hayakudumu kwa kuwa baadhi yetu tulikuwa tunayatumia kulima kwenye visiki, hii sio sawa, yatunzeni ili yale malengo tuliyoyakusudia ya kuendeleza sekta ya kilimo yaweze kutimia"
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeandaa mpango wa kuhifadhi maji yanayotiririka katika mabonde ya Mpumbe, Nanguruwe, Mnindu, na lililopo eneo la Lucas Malia ili yatumike kwa kilimo cha umwagiliaji.
Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt Hussein Mohamed Omary, amesema Ugawaji wa Matrekta hayo ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima.
Amesema katika awamu hiyo ya Kwanza kwa Wilaya ya Ruangwa wamekabidhi matrekta matano, majembe matano ya kulimia, vifaa vya kuchimbia na kusafisha mashamba na kifaa cha kuvunia mazao.
Amesema Katika awamu ya kwanza ya mpango huo Wizara ya Kilimo itaanzisha vituo 45 katika maeneo mbalimbali nchini.
"Lengo la Wizara ya Kilimo ni kugusa mnyororo mzima wa thamani ya mazao, na tutaendelea kutoa vifaa vingine kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija".
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma amesema kuwa matrekta hayo yatasaidia kuongeza eneo la kilimo hadi kufikia asilimia zaidi ya hamsini kutoka chini ya asilimia Thelathini ya sasa.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Frank Chonya amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Wilaya hiyo.
"Katika kipindi cha miaka minne Halmashauri imepokea zaidi ya Bilioni 45 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo Shilingi Bilioni tano zimeelekezwa katika sekta ya Kilimo".