Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Caspar Mmuya, amechukua rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Ruangwa, Mkoa wa Lindi, kupitia Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi zilizopo wilayani humo.
Tukio hilo limefanyika leo, Agosti 26, 2025, ambapo Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ruangwa, Mwalimu George Mbesigwe, alimkabidhi fomu hizo. Hatua hiyo imeashiria mwanzo wa safari mpya kwa Mmuya, ambaye baada ya utumishi wa muda mrefu serikalini sasa anaelekeza nguvu zake kwenye siasa za uwakilishi.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mmuya aliahidi kuendeleza na kusimamia utekelezaji wa mipango iliyoanzishwa na mtangulizi wake, akisisitiza dhamira yake ya kulitumikia Bunge kupitia wananchi wa Ruangwa.
Mmuya anatajwa kuwa na rekodi nzuri ya kiutendaji alipokuwa mtumishi wa umma, sifa zinazompa matumaini ya kuendeleza mchango wake kwa taifa kupitia nafasi ya ubunge.
Jimbo la Ruangwa lilikuwa likiwakilishwa na Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake, Kassim Majaliwa, ambaye hakutangaza nia yakugombea tena. Hatua ya Mmuya imeibua hamasa kubwa miongoni mwa wakazi wa Ruangwa, wakisubiri kwa shauku kuona nani ataibuka mshindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
