Na. Mwandishi Wetu, Lindi
Familia ya Bwana Majonde, inayodaiwa kuwa wamiliki wa ardhi inayopangwa kujengwa kituo cha Afya katika Kata ya Rutamba, imekubali kukaa katika meza ya mazungumzo na kamati ya Afya ya zahanati hiyo ili kutafuta suluhu. Hatua hii imefuatia ziara ya timu ya wataalamu wanaotoa msaada wa kisheria katika Kata hiyo, ambapo walitoa elimu ya kisheria, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Mgogoro huu ulijitokeza baada ya familia ya Bwana Majonde kudai kwamba sehemu ya kipande cha ardhi kinachotakiwa kutumika kwa ajili ya kituo cha Afya ni mali ya marehemu mzee wao. Walieleza kwamba wakati wa zoezi la upimaji wa eneo hilo, hawakushirikishwa, jambo lililosababisha familia kuanzisha taratibu za kuzuia ujenzi hadi taratibu za kisheria zitakapoheshimiwa, ikiwemo kushirikishwa katika hatua zote za upimaji.
Kabla ya kukubaliana kwa pande zote, Afisa Ardhi Mteule, Bw. Andrew Munisi, alikubaliana na pande zote mbili na kuwashauri kukaa pamoja kwa mazungumzo ili kutatua mgogoro huo na kuhakikisha mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya unaendelea.
Mjumbe wa kamati ya Afya ya zahanati hiyo, Bw. Bertram Thomas, alieleza umuhimu wa kituo hicho cha Afya kwa wakazi wa eneo hilo, na kuonyesha matumaini kwamba mgogoro huo utaisha ili ujenzi uendelee kama ilivyopangwa.