AZIMIO LA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA KUHUSU TANGAZO LA MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR LA KUITISHA UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi), likiwa ndiyo chombo cha juu cha maamuzi katika Chama baada ya Mkutano Mkuu wa Taifa, limefanya kikao cha dharura leo, tarehe 28 Januari, 2016, katika Ofisi Kuu ya CUF, mjini Dar es Salaam.
Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja tu, ambayo ni kufanya maamuzi kuhusiana na tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar la kuitisha uchaguzi wa marudio.
Baada ya kujadili kwa kina tamko hilo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, la kuitisha uchaguzi wa marudio tarehe 20 Machi, 2016 na mwenendo mzima wa hali ya kisiasa Zanzibar tokea alipotoa tamko lake batili la tarehe 28 Oktoba, 2015 kudai kwamba amefuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo yake, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:
1. KWAMBA Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar umeshafanyika tarehe 25 Oktoba, 2015, ambapo kwa upande wa uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani ulikwisha kamilika na washindi wote kupewa shahada za kuwathibitisha na kuwatambua kama washindi halali.
Kwa upande wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, matokeo yalikwisha bandikwa nje ya vituo vya majumuisho vya majimbo yote 54.
Kilichokuwa kinaendelea baada ya hapo ni kuhakiki matokeo hayo kutoka majimboni na kazi hiyo ilikwishakamilika kwa majimbo 40 na katika hayo, matokeo ya uchaguzi wa Rais kwa majimbo 31 yalikwishatangazwa kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salum Jecha, kutangaza isivyo halali kwamba ameufuta uchaguzi huo.
2. KWAMBA Chama Cha Wananchi (CUF) hakitoshiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 kwa sababu uchaguzi huo si halali kwani uchaguzi halali ulishafanyika.
3. KWAMBA linatoa wito kwa Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao na ambao wanaamini katika utawala wa sheria, demokrasia na kuheshimu Katiba na Sheria za nchi yetu kutoshiriki katika uchaguzi huo usio halali wa marudio.
4. KWAMBA sababu kuu ya Baraza Kuu kufikia maamuzi haya ni kutokana na matamko yote mawili ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, kutokuwa halali na kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.
Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio.
5. KWAMBA linazipongeza na limetiwa moyo sana na taasisi na jumuiya zote za kimataifa na kikanda zikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Madola (The Commonwealth), Umoja wa Ulaya (European Union), Umoja wa Afrika (African Union), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Marekani na Uingereza kwa msimamo wao wa kuungana na Wazanzibari na kutetea haki yao ya kidemokrasia na maamuzi halali waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kutaka mchakato wa uchaguzi huo ukamilishwe na matokeo yake kutangazwa.
6. KWAMBA linazipongeza na kutiwa moyo pia na taasisi za hapa nchini zikiwemo taasisi na jumuiya za kidini, taasisi za haki za binadamu, vyombo huru vya habari, vyama vyengine vya siasa na Wazanzibari na Watanzania wote wanaopenda amani na demokrasia kwa msimamo wao wa kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kuendelea kusisitiza haja ya kuheshimu na kufuata Katiba na Sheria za nchi yetu na pia haja na umuhimu wa kutunza amani ya nchi yetu kwa kutaka haki itendeke.
Baraza Kuu linazihakikishia taasisi na jumuiya hizo zote na pia kuwahakikishia Wazanzibari na Watanzania wote kwamba CUF itaendelea kusimama kidete katika kulinda na kutetea Katiba na Sheria za nchi yetu na pia kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015.
7. KWAMBA limesikitishwa na kushangazwa na kitendo cha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuandika barua na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kutaka vyama vya siasa vishiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 bila ya kujali kwamba uchaguzi huo ni haramu na unakiuka matakwa ya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.
Baraza Kuu halikutarajia mtu mwenye hadhi ya Ujaji kufanya kazi ya kutumikia maslahi ya watawala ambao wameamua kuvunja Katiba na Sheria za nchi yetu na kukanyanga misingi ya haki na demokrasia huku akishindwa kukemea uhuni mkubwa uliofanywa wa kubaka demokrasia na haki za watu.
8. KWAMBA limesikitishwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, kukwepa dhamana na wajibu wake kama Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuiacha njiani kazi aliyoianza ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo wa uchaguzi Zanzibar.
Baraza Kuu linamtaka Rais Magufuli kujitathmini na kujiuliza anajiweka vipi na kutoa taswira gani mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa kutokana na kutosimamia ahadi yake aliyoitoa mbele ya Watanzania wakati akilizindua Bunge jipya kwamba atafanya kazi na vyama vya CUF na CCM ili kuupatia ufumbuzi mkwamo huu.
9. KWAMBA linalaani matumizi ya nguvu kubwa ya vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano na Vikosi vya SMZ dhidi ya wananchi wasio na hatia na ambao wamekuwa watulivu licha ya vitendo vingi vya uchokozi wa makusudi na hata mashambulizi ya hujuma dhidi yao yanayofanywa na makundi ya vijana wa CCM waliowekwa katika makambi kadhaa kisiwani Unguja.
10. KWAMBA linaitaka jumuiya ya kimataifa na hasa taasisi zinazosimamia haki za binadamu na zinazopambana na makosa ya jinai kimataifa ikiwemo Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (International Criminal Court – ICC) kufanya uchunguzi wa kauli na matendo ya uhalifu, uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu na ubaguzi ambao umekuwa ukifanywa dhidi ya wananchi wa Zanzibar na kuchukua hatua dhidi ya watu walio nyuma ya maamuzi na utekelezaji wa matukio hayo.
11. KWAMBA linawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu na kuwa watulivu licha ya machungu makubwa waliyoyapitia na wanayoendelea kuyapitia tokea pale maamuzi yao yalipopinduliwa na CCM kwa kumtumia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha.
Baraza Kuu linatoa wito kwa Wazanzibari wote kuungana pamoja chini ya chama chao cha CUF walichokipa ridhaa halali kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 kutetea maamuzi yao waliyoyafanya kupitia sanduku la kura kwa njia za amani.
Baraza Kuu linawasisitiza tena Wazanzibari kwamba waendelee kutunza amani ya nchi yetu na kutambua kwamba kutunza amani si udhaifu bali ni jambo linaloipa nguvu jumuiya ya kimataifa kufuatilia haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar.
12. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawatahadharisha CCM na watawala wasiowajali na kuwaheshimu wananchi kwamba zama za utawala wa mabavu usioheshimu Katiba na Sheria za nchi hazina nafasi tena katika dunia ya leo. Baraza Kuu lina imani kwamba HAKI ITASHINDA.
LIMETOLEWA NA:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi)
DAR ES SALAAM
28 JANUARI, 2016.