Stars imetoka sare ya kutofungana bao lolote na Burundi katika mechi ya raundi ya pili iliyochezwa katika uwanja wa taifa ya Nyayo mjini Nairobi.
Kenya ilishindwa kuilaza Burundi licha ya kuwa na wachezaji kumi pekee baada ya mechezaji wake mmoja kupewa kadi nyekundu wakati wa mechi hiyo.
Timu hiyo ya Kenya itajilaumu kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga lakini wakosoaji wasema Stars ilikosa kufanya vyema kutokana na maandalizi mabaya.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Henri Michel kutoka Ufaransa alijiuzulu na kuondoka bila kwa heri na hivyo kuiacha timu hiyo bila mkufunzi kwa muda.
Timu hiyo ya Kenya imekuwa chini ya uongozi wa kaimu kocha mkuu James Nandwa ambaye aliongoza kikosi hicho kufika fainali ya kuwania kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA, mjini Kampala, Uganda.
Kufikia wakati wa mapumziko hakuna timu iliyokuwa imeona lango la mwenzio.
Ratiba ya raundi ya mwisho
Burundi sasa itachuana na Sudan mwezi Juni kwa raundi ya mwisho.
Timu itakayoshinda itafuzu kwa fainali za mashindano hayo ya CHAN yatakayofanyika Afrika Kusini mwakani.Mechi zingine za kanda ya Afrika Mashariki ni mshindi kati ya Eritrea na Ethiopia atakutana na Rwanda huku Uganda ikipambana na Tanzania kuamua watakaosafiri Afrika Kusini.
Bingwa mtetezi wa mashindano ya pili ya CHAN yaliyofanyika mwaka wa 2011 nchini Sudan ni Tunisia iliyoshinda Angola 3-0 mechi ya fainali mjini Khartoum.
Sudan ilimaliza ya tatu kwa kushinda Algeria 1-0 mechi ya kuamua mshindi wa tatu.
Mashindano ya kwanza ya CHAN yalifanyika mwaka wa 2009 na katika mechi ya fainali DR Congo ilishinda Ghana 2-0 kwenye mechi ya fainali mjini Abidjan.