NIJUZE NIJUZE Author
Title: TAARIFA YA WIZARA YA AFYA KUHUSU UGONJWA WA EBOLA MKOANI KAGERA
Author: NIJUZE
Rating 5 of 5 Des:
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye vyombo mbal...
mohSW Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye vyombo mbali mbali vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani Karagwe mkoa wa  Kagera.
Mnamo tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na Ustawi Wa Jamii ilipokea taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya kuwepo kwa mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola, katika hospitali ya Wilaya ya Nyakahanga. Aidha,taarifa hiyo ilibainisha kuwa mgonjwa huyo alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka (6|) kutoka katika kijiji cha Nyakatundu wilayani Karagwe. Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali, kulegea, kutokwa damu puani, kutapika damu, na kukojoa damu.Maelezo kutoka kwa mama mzazi zilieleza kuwa mtoto huyu alianza kuugua kuanzia tarehe 30 Agosti 2012, ambapo alipatiwa dawa ya Septrin baada ya hospitali binafsi kuonyesha kuwa ana  ugonjwa wa“Typhoid”.
Uchunguzi wa awali katika hospitali ya Nyakahanga ulionyesha kuwa mtoto huyu alikuwa anasumbuliwa na uambukizo kwenye haja ndogo (Urinary Tract Infection).Vile vile alifanyiwa uchunguzi wa kimaabara na Vipimo vya malaria, Hepatitis na Typhoid havikuonyesha kuwepo kwa magonjwa haya. Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka mgonjwa na mama yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa ajili ya uangalizi zaidi.
Aidha mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Kagera imeweza kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina pamoja na kuchukua sampuli za damu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika maabara ya Taifa ya uchunguzi wa magonjwa na Maabara za nje ya nchi, ili kubaini kama ameathirika na ugonjwa wa Ebola. Timu hiyo ya wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya mgonjwa huyu kwa sasa imeimarika ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na kukojoa damu kumekoma pia, uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha kuwa hana dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.Vile vile hakuna taarifa ya mtu mwingine yeyote kwenye familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au cha jirani kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;
· Imepeleka timu ya wataalamu mbali mbali kutoka Wizarani na mkoa kwa lengo la kwenda kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo.
· Imetoa elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea ugonjwa wa Ebola pamoja na dalili za ugonjwa huu, kwa wananchi na watumishi wa afya katika hospitali   ya Nyakahanga
· Kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya Nyakahanga pamoja na maeneo ya mipakani
· Kutoa matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza sauti na kupitia radioni (Radio Karagwe) kuhusu ugonjwa huu.  Aidha, vipeperushi pia vimetolewa.
Hitimisho
Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa nchini.Aidha, Wizara ya Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu iwapo utatokea hapa nchini.
Kwa sasa timu za wataalum zipo katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha, kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa wataalamu na kwa wananchi na vilevile kufuatilia ugonjwa huu sehemu za mipakani.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa haraka kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za afya, mara wanapoona dalili za ugonjwa huu.

Imetolewa na:

kitengo cha Mawasiliano

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii

Tarehe 6 Agosti, 2012














About Author

Advertisement

 
Top