Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha,
Bw. Salim Khalfan Kimaro, akitoa elimu ya fedha kwa wakazi wa Ganyange
Wilayani Tarime, Mara, ambapo aliwataka kuwafichua watoa huduma ndogo za
fedha wanaofanya kazi kinyume na Sheria, wakati wa zoezi la kutoa elimu
hiyo mkoani Mara.
Afisa Masoko Mwandamizi wa Kampuni ya Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim
Mwanga, akieleza umuhimu wa kuwekeza katika Mifuko ya Kampuni hiyo,
wakati wa zoezi la kutoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Tarime Mkoani
Mara.
Wakazi wa Nyasincha, Mbogi, Pemba na Ganyange Wilayani Tarime wakipata elimu ya fedha inayotolewa
bure na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha
ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro, katika zoezi la utoaji wa elimu
hiyo Mkoa wa Mara.
Na. Peter Haule, Tarime, Mara, WF.
Kiongozi
wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw.
Salim Khalfan Kimaro amewataka wakazi wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara,
kutoa taarifa kwa Mamlaka husika inapobainika uwepo wa mtoa huduma
ndogo za fedha asiyesajiliwa na anayetoa huduma kinyume cha Sheria.
Rai
hiyo imetolewa wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha katika maeneo
ya Manga, Sirari, Matombo, Nyamwaga, Ganyange na Gorong’a, yaliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Bw.
Kimaro alisema kuwa uwepo wa watoa huduma ya fedha wasiosahihi
wanachangia kwa kiasi kikubwa kufifisha maendeleo ya wananchi jambo
ambalo Serikali haiwezi kulifumbia macho.
“Tumekuja
kutoa elimu, tunafanya kwa jitihada kubwa kuhakikisha kwanza wananchi
wanauelewa wa masuala ya fedha, wanatambua haki zao wakati wa kupata
huduma za fedha na pia kuwa na uwezo wa kutambua huduma iliyosahihi na
isiyosahihi ili waweze kuchukua hatua ikiwemo kupeleka taarifa katika
Mamlaka husika pale inapobainika kunachangamoto ya watoa huduma hao”,
alisema Bw. Kimaro.
Aidha, aliwataka wananchi
kusimamia fedha zao na kuepuka kufanya sherehe au ngoma na mambo mengine
yasiyokuwa ya maendeleo wanapopata fedha zinazotokana na shughuli zao
halali za kiuchumi na badala yake wajiwekee akiba maeneo yenye tija kama
vile Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja na Hati fungani za Serikali.
Bw.
Kimaro alisema kuwa Utafiti wa FinScope wa mwaka 2023 nchini, unaeleza
kuwa ni asilimia 53.5 tu ya nguvukazi ndiyo waliotumia huduma rasmi za
fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la Watanzania ambao hawafaidiki na
huduma hizo na hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia
shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema kuwa
Programu ya Elimu ya Fedha kwa umma ilianza Mei, 2024, na hadi sasa
mikoa 15 imefikiwa na uelekeo ni Mkoa wa Mwanza ambao anaamini watu
wengi zaidi watajitokeza kupata elimu ya fedha kwa manufaa ya maisha
yao.
Tags
HABARI ZA KITAIFA