Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari
(JAB), imeweka bayana msimamo wa kisheria wa Sheria ya Huduma za Habari
kuwa kipaji pekee hakitoshi kumfanya mtu afanye kazi za kihabari kama
hajapitia katika taaluma ya Uandishi wa Habari na kukidhi vigezo.
Msimamo
huo umebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Wakili Patrick
Kipangula leo Jumatatu tarehe 17 Machi, 2025 jijini Dar es Saalam,
wakati akizungumza katika kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na
Radio One na kujibu swali la mmoja wa wasikilizaji aliyetaka kujua
mamlaka ya Bodi katika kushughulikia walio kinyume cha sheria.
Wakili
Kipangula amesema kama Serikali na nchi kwa ujumla imekubali kwamba
Uandishi wa Habari ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine ni lazima
kufuata matakwa ya kisheria.
Amesema kuwa hata kama mtu ana
kipaji kikubwa kiasi gani, kama hajasoma taaluma ya uandishi wa habari
haruhusiwi kisheria kufanya kazi za kihabari.
"Kifungu cha 19
(1) cha Sheria ya Huduma za Habari, kinasema ‘Mtu hataruhusiwa kufanya
kazi ya Uandishi wa Habari, isipokuwa mtu huyo awe amethibitishwa kwa
mujibu wa masharti ya Sheria", amesema Wakili Kipangula na kuongeza.
“Sisi
Bodi, tunawashauri na kuwasisitiza wale wote wanaofanya kazi za
kihabari bila kuwa na sifa waende shule, wakimaliza watarudi kuendelea
na taaluma yao, uzuri ni kwamba mtu kama ana Shahada ya Udaktari
anaruhusiwa kusoma Diploma (Stashahada) tu ya Uandishi wa Habari, na
huyu anaweza kuwa mwandishi mzuri wa habari za afya,”.
Amesisitiza
kuwa Serikali kupitia Waziri mwenye Dhama na Habari wakati huo,
ilishatoa muda wa ziada wa miaka mitano ili wale waliokuwa hawakuwa
wamesoma warudi shule wakasome, na ulipoisha aliongeza tena mwaka mmoja.
Akijibu swali kuhusu wajibu wa chombo cha habari katika suala
la mtangazaji au mwandishi kufanya kazi za kihabari bila kusomea
taaluma, Wakili Kipangula amesema chombo cha Habari kina wajibu wa
kuajiri watumishi/waandishi waliotimiza vigezo vya kitaaluma kwa mujibu
wa Sheria.
