BEI YA MBAAZI YA PANDA MRAJIS ATOA MSIMAMO WA SERIKALI

Na Ahmad Mmow, Nachingwea

Mnada wa nne wa mbaazi msimu wa 2025 umefanyika leo kijijini Mpiruka B, wilayani Nachingwea, na kushuhudia bei ya juu ikipanda hadi shilingi 790 na ya chini shilingi 730 kwa kilo moja. Jumla ya kilo 4,465,465 zimeuzwa katika mnada huo kupitia chama cha msingi cha ushirika cha Ukombozi AMCOS.

Hii ni tofauti na mnada wa tatu uliofanyika Liwale, ambapo bei ilikuwa kati ya shilingi 640 – 680 kwa kilo moja.

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Lindi, Kenneth Shemdoe, alisema serikali bado iko wazi kwa usajili wa vyama vipya vya ushirika, lakini kwa masharti ya kufuata sheria, kanuni na taratibu husika. Alibainisha kuwa lengo ni kuwa na vyama imara na vyenye tija, hivyo vyama visivyo na uwezo vitaunganishwa au kufutwa, huku vinavyoonyesha uhitaji na sifa sahihi vikitambuliwa rasmi.

Shemdoe aliwataka viongozi wa AMCOS kusimamia vyema vyama vyao ili viwe na miradi ya kiuchumi itakayotoa ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla.

Aidha, akizungumzia maandalizi ya msimu wa 2024/2025 wa zao la korosho, aliwaonya wakulima kuhakikisha ubora wa mazao yao kuanzia hatua za upandaji, palizi hadi uhifadhi, akisisitiza kuwa ubora ndio utakaowezesha kupata soko la uhakika.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post