RUANGWA HATUNA DENI NA RAIS DKT. SAMIA - MAJALIWA

Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wakazi wa Wilaya ya Ruangwa hawana deni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa aliyoifanya wilayani humo.


Amesema Rais Dkt. Samia ametoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta za kilimo, afya, elimu, miundombinu na nyinginezo.


Ameyasema hayo Jumamosi, 15 Machi 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wanakijiji wa kijiji cha Narungombe, Wilayani Ruangwa.


"Rais Dkt. Samia amewezesha kupatikana kwa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo nchini ikiwemo kwenye wilaya yetu ya Ruangwa, Tunaachaje kumuunga mkono kwa kazi kubwa aliyoifanya."


Amesema Wana-Ruangwa wanatoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyotoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.


"Wilaya yetu ilikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji kutokana na kuwa na chumvi nyingi chini inayotokana na sababu za kijiografia lakini Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana."


Amesema Serikali iko katika hatua za utekelezaji za mradi mkubwa wa maji  wa shilingi bilioni 119 kutoka mto Nyangao, kuja vijiji 34 vya Ruangwa ambao utahakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika wilayani humo.


"Nitaendelea kufanya kazi na nyie usiku na mchana, jua kwa mvua hadi kuhakikisha Ruangwa inafanikiwa zaidi".

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post