Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga akizungumza na wakazi wa kata wa Mang’oto Wilayani Makete Mkoani Njombe wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ya kukagua miradi ya usambazaji wa umeme, tarehe 17 Machi 2025.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini, Mhe. Mathayo David (Katikati) akizungumza jambo wakati wa ziara ya
kukagua miradi ya usambazaji wa umeme
katika Kata ya Mang’oto, wilayani Makete mkoani Njombe, tarehe 17 Machi 2025.Kulia
ni Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith
Kapinga.Na. Mwandishi Wetu, Njombe
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kubandika gharama halisi za kuunganishiwa umeme pamoja na taratibu za kufuata kwa wananchi wanapotaka kuunganishiwa umeme katika Ofisi za Serikali za Vijiji. Hatua hii inalenga kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi na za ufanisi kabla ya kufanya maombi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Mathayo David, katika ziara ya kukagua miradi ya usambazaji wa umeme iliyofanyika tarehe 17 Machi 2025 katika Kata ya Mang’oto, wilayani Makete mkoani Njombe.
Mhe. Mathayo alisisitiza kuwa ili kuondoa mkanganyiko wa wananchi kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme, ni muhimu kwa TANESCO na REA kubandika taarifa za gharama na hatua zinazohitajika kwa uwazi katika Ofisi za Serikali za Vijiji. Alieleza kuwa wananchi wengi, hasa vijijini, wamekuwa na hofu kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme kwa sababu ya kukosa taarifa sahihi, jambo ambalo linaongeza changamoto katika kupata huduma hiyo.
“Wananchi wameshindwa kujua gharama halisi za kuunganishiwa umeme na hii inawapa hofu wanapohitaji huduma. Kama taarifa zitakuwa wazi, itasaidia kupunguza mkanganyiko na kuondoa kikwazo cha wananchi kwenda ofisi za TANESCO kupata maelezo,” alisema Mhe. Mathayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, aliwataka REA na TANESCO kuongeza juhudi katika kuwahamasisha wananchi kuunganishiwa umeme, akisisitiza umuhimu wa kusuka nyaya katika nyumba za wananchi kabla ya miradi ya umeme kukamilika ili wengi wapate huduma hiyo. Aliwahimiza pia wananchi kutumia namba ya huduma bure ya 180 kwa ajili ya kutatua changamoto zao kwa haraka.
Wananchi wa Mang'oto walieleza furaha yao kwa kupata umeme, kwani awali walikuwa wakilazimika kwenda vijiji jirani kufuata huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kusaga nafaka na kupata huduma za chanjo katika zahanati zenye umeme.
Ziara hii ilihusisha viongozi wakuu kutoka Wizara ya Nishati, ikiwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Khatib Kazungu, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, pamoja na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara na maafisa wengine.


