Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo,
akimkabidhi zawadi Mkurugenzi Msaidizi Idara inayosimamia Afrika,
Mashariki ya Kati na Latin America wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland,
Bi. Helena Airaksinen, baada ya majadiliano ya tathmini ya utekelezaji
miradi inayofadhiliwa na nchi hiyo nchini, majadiliano yaliyofanyika,
Treasury Square, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo,
akizungumza kuhusu miradi inayofadhiliwa na Finland, alipokutana na
kufanya mazungumzo na na Mkurugenzi Msaidizi Idara inayosimamia Afrika,
Mashariki ya Kati na Latin America wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland,
Bi. Helena Airaksinen (wa pili kulia), ulioambatana na Balozi wa nchi
hiyo Tanzania, Mhe. Theresa Zitting (wa kwanza kulia), walipofika
ofisini kwake, Treasury Square, jijini Dodoma.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi.
Jenifa Christian Omolo, na Ujumbe wa Finland ukiongozwa na Mkurugenzi
Msaidizi Idara inayosimamia Afrika, Mashariki ya Kati na Latin America
wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Helena Airaksinen wakiwa
katika picha ya pamoja baada ya majadiliano ya tathmini ya miradi
inayofadhiliwa na Finland, yaliyofanyika jijini Dodoma.
Na. Peter Haule, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, amekutana na kufanya
mazungumzo na ujumbe kutoka Finland ukiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara inayosimamia Afrika, Mashariki ya Kati na Latin America wa Wizara
ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Helena Airaksinen, ulioambatana na
Balozi wa nchi hiyo hapa nchini, Mhe. Theresa Zitting.
Akizungumza
katika mkutano huo, Bi. Omolo alisema kuwa, ujumbe huo umekuja kwa
lengo la kufanya tathmini ya kiutendaji wa shughuli mbalimbali za
maendeleo zilizotekelezwa kupitia msaada wa nchi hiyo kwa kipindi cha
mwaka 2021 hadi 2024 ili kupanga mikakati mingine kwa mwaka 2024 hadi
2028.
Alisema kuwa tangu mwaka 2010 Finland ilitoa
kiasi cha Euro zaidi ya milioni 351 ili kutekeleza miradi mbalimbali
ambayo imekamilika kwa takribani asilimia 87 na asilimia 13 ya miradi
hiyo bado ipo katika hatua ya utekelezaji.
“Makubaliano
ya ushirikiano wa kimaendeleo wa hivi karibuni kati ya nchi hizi mbili
ulijikita kutekeleza program za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuimarisha
masuala ya uchumi, kuhamasisha kutengeneza ajira, eneo la ubunifu,
kujenga uwezo kuhusu kodi na utawala bora katika kipindi cha mwaka 2021
hadi 2024”, alisema Bi. Omolo.
Alisema kuwa
kutokana na program kumalizika mwaka 2024 ni dhahiri kunahitajika
majadiliano yatakayowezesha kuwa na program mpya zinazotakiwa
kutekelezwa kuanzia mwaka 2025.
Alisema katika
majadiliano hayo Timu za Wataalamu kutoka pande mbili zitaainisha maeneo
mapya ya ushirikiano kulingana na Dira ya Taifa ili yaweze kufanyiwa
kazi na wadau hao wa maendeleo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Msaidizi Idara inayosimamia Afrika, Mashariki ya Kati na
Latin America wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Helena
Airaksinen, alisema kuwa maeneo ya ushirikiano kati ya nchi yake na
Tanzania yameendelea kuongezeka licha ya kubadilishwa kwa Sera za nchi.
Alisema
kuwa zipo nchi nyingi ambazo zimeondolewa katika utekelezaji wa program
kupitia nchi yake lakini Tanzania itaendelea kuwa mshirika muhimu
katika kuchochea maendeleo ya pande hizo mbili kutoka na juhudi zake
katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Majadiliano
kati ya pande hizo mbili yalihusisha pia wajumbe kutoka Wizara ya
Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maendeleo
ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia, Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki na Tume ya Mipango.
Tags
HABARI ZA KITAIFA