Na. Mwandishi Wetu, Nachingwea
Chama Kikuu cha Ushirika cha Ruangwa, Nachingwea na Liwale (RUNALI) kimekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni arobaini na nne na laki saba (44,700,000.00) kwa hospitali za wilaya tatu, ambazo ni wanachama wa chama hicho. Vifaa hivyo vinajumuisha mashine za ultrasound na vifaa maalum kwa ajili ya watoto njiti, ambapo kila wilaya imepata vifaa vyake.
Mwenyekiti wa chama hicho, Ndg. Odas Mpunga, amesema kuwa lengo la kukabidhi vifaa hivyo ni kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, hasa kwa watoto njiti na wajawazito. Aliongeza kuwa RUNALI imekuwa ikiweka mkazo katika kurudisha faida kwa jamii, na hivyo wameamua kusaidia hospitali za wilaya hizo ili kuboresha huduma za afya.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo, ambaye alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, aliwasihi wauguzi na viongozi wa hospitali kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinatumika kwa ufanisi ili wananchi waweze kupata huduma bora. Alisisitiza pia umuhimu wa wahudumu wa afya kuwahudumia wagonjwa kwa upendo, heshima, na lugha nzuri ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.