WANANCHI LINDI WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KUANDIKA WOSIA

 Afisa Aridhi Mteule wa Manispaa ya Lindi na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria Andrew Munisi akitoa elimu kwa wananchi waliojitokeza kusikiliza kampeni ya msaada wa Kisheria
Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria

Na Mwandishi Wetu, Lindi

Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, mkoani Lindi, wametakiwa kuachana na dhana potofu ya kuhusisha wosia na uchuro, na badala yake kufanya hivyo kama njia ya kuepusha migogoro ya mali baada ya kifo.

Hayo yamesemwa na Afisa Aridhi Mteule wa Manispaa ya Lindi na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria, wakati alipozungumza na wananchi wa vijiji vya Moka, Likwaya, na Matimba, leo Februari 23, 2025.

Afisa huyo, Munisi, alisema kuwa watu wengi wamekuwa na mtazamo potofu kwamba wosia ni jambo la uchuro au lina uhusiano na kifo, jambo ambalo si sahihi. Alisisitiza kwamba wosia ni muhimu ili kuhakikisha mali ya familia inagawiwa kwa haki na usawa baada ya kifo cha mmiliki.

Aidha, alifafanua faida za kuwa na wosia, ikiwa ni pamoja na kuepuka migogoro ya kifamilia, kulinda haki za watoto, na kuweka mipango bora ya kifamilia. Alizitaja pia hatua muhimu za kuzingatia wakati wa kuandika wosia, ikiwa ni pamoja na kutafuta ushauri wa kisheria, kuhakikisha wosia umeandikwa kwa mujibu wa sheria, na kuliwekwa saini na mashahidi waliothibitishwa ili kuthibitisha uhalali wake.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri hiyo, Bwana Kasimu Mkwili, alisema kuwa wosia unamruhusu marehemu kumtambua mtoto hata akiwa amezaliwa nje ya ndoa, jambo ambalo linawasaidia watoto kutambulika na kurithi mali za familia. Alitoa mfano wa sheria za dini ya Kiislamu ambapo mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa hawezi kutambulika kama mtoto wa marehemu, lakini kupitia wosia, mtoto huyo anaweza kurithi mali za mzazi wake hata kama hakutambulika kabla ya kifo.

Bwana Juma Mbarouk, mkazi wa Moka, alisema wananchi wamefurahi kwa kupata elimu hii na wamejifunza mambo mengi kuhusu wosia na masuala mengine ya kisheria kutoka kwa timu ya wataalamu wa msaada wa kisheria.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post