Na. Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Mchezo wa Ligi Kuu kati ya Simba na Azam FC uliofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa umemalizika kwa sare ya 2-2.
Huu ulikuwa ni Mzizima Derby, mechi yenye ushindani mkubwa kutoka kwa kila timu. Simba walitawala mchezo kwa ujumla, huku Azam FC wakitekeleza mashambulizi ya kushitukiza.
Azam FC walikuwa wa kwanza kupata bao la uongozi dakika ya kwanza kupitia kwa Gibril Sillah, aliyemalizia shambulizi la kushitukiza.
Simba walijibu mapema dakika ya 25 kupitia kwa Elie Mpanzu, ambaye alifunga baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Kibu Denis.
Kipindi cha pili kilikuwa cha upinzani mkali, ambapo Simba walifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 76. Abdulrazak Hamza alifunga kwa kichwa baada ya mpira wa adhabu uliochapwa na Jean Charles Ahoua.
Hata hivyo, Azam FC walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika mbili kabla ya kumalizika kwa mchezo. Zidane Sereli alifunga kwa pasi nzuri kutoka kwa Feisal Salum, baada ya kumzidi mbio nahodha wa Simba, Mohammed Hussein 'Zimbwe Jr'.