BOT: FAIDA LUKUKI KUUZA DHAHABU

Madini ya dhahabu

Na. Salome Kitomari. Nipashe

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuwa tangu kuanzishwa kwa mpango wa kununua dhahabu, tayari imenunua tani mbili, na lengo lake ni kufikia tani sita zenye thamani ya Dola za Marekani 350.

Dunga Nginela, mchambuzi wa masuala ya kifedha wa BoT, alielezea umuhimu wa mpango huu kwa waandishi wa habari mjini Mtwara, akisema mafanikio hayo yametokana na motisha iliyowekwa kwa wachimbaji. Aliongeza kuwa baada ya kutangaza mpango wa ununuzi wa dhahabu, mwitikio wa wachimbaji ulikuwa mdogo, hivyo BoT ililazimika kutoa motisha kama kupunguza mrabaha, kutoa bei nzuri ya kununua dhahabu, na kutoa msamaha wa VAT.

Nginela alibainisha kuwa changamoto kubwa ni kwamba wengi wa wachimbaji wana mikataba na watu wa nje ya nchi, jambo ambalo BoT hailinganii nalo. Ili kushughulikia hilo, BoT ilianzisha utaratibu wa kuvutia wachimbaji kwa kutoa nyaraka fupi na kujenga uhusiano mzuri na viwanda vya kuchenjua dhahabu.

Akaongeza kuwa dhahabu ni muhimu kwa uchumi wa taifa, kwani inachangia kwa kiwango kikubwa, ingawa sehemu kubwa yake huchenjuliwa nje ya nchi. Alisema dhahabu inathaminiwa kimataifa na inaweza kutumika kama akiba, tofauti na fedha za kawaida. Kwa mfano, dhahabu ina bima ambayo fedha haina, na inatumika kama njia ya kudhibiti vita, mfano ni jinsi Urusi ilivyokuwa ikinunua dhahabu kwa muda mrefu, huku Marekani ikifanya hivyo ili kudhibiti mabadiliko katika matumizi ya fedha.

Nginela aliongeza kuwa bei ya dhahabu inakua kwa kasi kutokana na uhaba wake, na inatarajiwa kupanda zaidi kwa kuwa inaaminika kuwa itaisha. Alisema kuwa dhahabu ina manufaa maalum, na mara nyingi bei yake hupanda hasa wakati wa misukosuko kama vita na janga la COVID-19, ambapo wawekezaji wengi hununua dhahabu ili kutunza mali zao.

Ofisa huyo alisisitiza kuwa dhahabu inayonunuliwa na BoT ni ya Tanzania, kwani inanunuliwa kwa fedha za ndani, na kwamba mpango huu unalenga kuongeza akiba ya dhahabu, kutofautisha akiba za fedha, na kukuza sekta ya uchimbaji madini ya ndani. Alisema awali walikuwa wakikumbana na changamoto ya wachimbaji kutopenda mchakato wa kisheria, lakini sasa wamefanikiwa kubadili mtindo wa kufanya biashara kupitia masoko ya dhahabu.

Akaongeza kuwa BoT inaendelea kununua dhahabu moja kwa moja kutoka kwa wachimbaji na madalali, na kwamba tangu Oktoba 2024 walianza kununua dhahabu kutoka kwa viwanda vitatu vya kuchenjua dhahabu vilivyopo Geita, Mwanza, na Dodoma, ambapo dhahabu ya Tanzania huchenjuliwa kutoka asilimia 80 hadi 90 na kufikia kiwango cha juu cha asilimia 99.5.

Kwa upande wa bei, Nginela alifafanua kuwa bei ya dhahabu inajulikana duniani kote kwa kuwa kuna minada miwili kila siku ambayo inatoa bei halisi ya dhahabu. Alisema mara dhahabu itakapokabidhiwa kiwandani na kupitishwa na BoT, malipo hufanyika ndani ya saa 24.

Aidha, alisema BoT haikusudii kuua soko la dhahabu nchini, na ndio maana wameweka utaratibu mzuri wa kununua kupitia madalali ambao wanachambua masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kuhusu umuhimu wa akiba ya fedha za kigeni, Nginela alisisitiza kuwa inachangia katika uthabiti wa uchumi kwa kuimarisha sarafu ya nchi na kusaidia utekelezaji wa sera ya fedha. Pia alisema akiba ya dhahabu husaidia kama kinga wakati wa migogoro ya kiuchumi au misukosuko ya nje, na kuwa ni ishara ya nguvu za kiuchumi kwa wawekezaji.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post