NIJUZE NIJUZE Author
Title: MAMA SAMIA LEGAL AID YAFIKIA WANANCHI ZAIDI YA MILIONI 1
Author: NIJUZE
Rating 5 of 5 Des:
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameeleza kuwa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni wazo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ...

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameeleza kuwa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni wazo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan linalolenga kuongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi wasioweza kumudu gharama za huduma za kisheria.

Amesema kuwa kupitia kampeni hii, ambayo inatolewa bure, zaidi ya wananchi milioni moja wamefikiwa hadi sasa, wakiwemo wanawake 681,326 na wanaume 691,773 kutoka mikoa 19 ya Tanzania.

Waziri Mkuu aliyasema hayo leo Jumatano (Februari 19, 2025), wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika mkoa wa Lindi, viwanja vya Madini, Ruangwa.

“Dkt. Samia aliona changamoto zinazowakumba Watanzania, hasa wale wasioweza kulipia huduma za kisheria, na aliguswa na alijua ni jambo muhimu kuwasaidia. Alianza kampeni hii na kuikabidhi Wizara ya Katiba na Sheria kusimamia utekelezaji wake,” alisema Majaliwa.

Ameongeza kuwa kupitia kampeni hii, migogoro ya ardhi, ndoa, na mirathi imeweza kutatuliwa. Ameeleza kuwa, migogoro ya mirathi imekuwa ni changamoto kubwa katika jamii nyingi, ikichangia uvunjifu wa amani miongoni mwa familia na ndugu.


Vilevile, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wakuu wa wilaya kote nchini kuanzisha ziara za kusikiliza na kutatua kero za kisheria za wananchi, badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa wafanye ziara. “Watanzania wanahitaji huduma hii ya Serikali, na Serikali imejizatiti kutoa huduma bora, tutaendelea kutumikia wananchi,” aliongeza.

Waziri Majaliwa alisema kuwa Rais Dkt. Samia ameleta mageuzi makubwa katika sekta ya sheria, akipa kipaumbele kutatua changamoto zinazozikabili. Aidha, aliiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuandika na kutunza wosia na kugawa mirathi kwa mujibu wa sheria ili kupunguza migogoro katika familia.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema kuwa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ina sifa nne kuu: umuhimu wake kwa jamii, umaalum wake kwa kuwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia, umahususi wake kwa kuwa ni wazo la Rais, na umakini wake kwa kutekeleza falsafa ya R4.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, alisema kuwa Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati na kwa ufanisi. Aliongeza kuwa, ili kufanikisha lengo hili, Wizara inaendelea kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria na kujenga uwezo kwa watoa huduma za msaada wa kisheria ili kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.

"Mwezi Desemba, 2024, Wizara ilingia makubaliano na Chama cha Wanasheria Tanganyika ili kuimarisha huduma za uwakili kwa wananchi wasioweza kumudu gharama za mawakili," alisema Naibu Waziri Sagini.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top