Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV) zinapatikana bure kwa WAVIU wote.
Dkt. Mollel ametoa kauli hiyo Februari 20, 2025, wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya Mradi wa Timiza Malengo mkoani Lindi, uliozinduliwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Deriananga, kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.
![]() |
Pichani, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Deriananga, wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya Mradi wa Timiza Malengo mkoani Lindi kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa. |
Mhe. Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha sekta ya afya kwa
kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya
afya pamoja na upatikanaji wa dawa zikiwemo dawa za kufubaza virusi vya
UKIWMI (ARV)
"Serikali imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 48 kwa
ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya, ikiwa ni pamoja na hospitali,
vituo vya afya na zahanati katika mkoa wa Lindi na maeneo mengine
nchini," amesema Dkt Mollel
Aidha, Dkt. Mollel amesisitiza kwamba
Serikali itaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha kwamba huduma za
afya zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi, huku akiwahimiza wananchi
kuwa na utamaduni wa kupima afya zao ili kuepuka magonjwa yanayoweza
kuzuilika.
Pia, Dkt. Mollel amesema kwa sasa huduma za kibingwa,
ikiwemo matibabu ya uvimbe wa ubongo bila kupasua kichwa na matibabu ya
kansa ya ubongo kwa kutumia sauti maalum, zinapatikana nchini Tanzania
ambapo upatikanaji wa huduma hizo za kibingwa hapo awali zilikuwa
zikipatikana kwa shida au kutoonekana kabisa.
Mradi wa Timiza
Malengo awamu ya tatu unalenga kuboresha sekta ya afya na unasimamiwa
katika halmashauri 36 za mikoa 10 ya Tanzania Bara, ambapo mikoa ya
Dodoma, Geita, Lindi, Mara, Morogoro, Njombe, Ruvuma, Singida, Tabora,
na Tanga inahusika.
Mradi huu unalenga kuhakikisha upatikanaji wa
huduma bora za afya na kuboresha mazingira ya huduma za afya kwa
wananchi wote, huku Serikali ikijitahidi kutekeleza malengo ya kuleta
maendeleo kwa wananchi, hasa wale walioko maeneo ya vijijini.