GLOBAL PEACE FOUNDATION YAZINDUA MRADI WA JAMII SHIRIKISHI KATIKA UZALENDO NA ULINZI

Shirika la Global Peace Foundation limetangaza rasmi uzinduzi wa mradi wa Jamii Shirikishi katika Uzalendo na Ulinzi katika kanda ya Kusini. Hafla ya uzinduzi ilifanyika leo, tarehe 18 Februari 2025, mkoani Lindi, kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali na udhamini wa Ubalozi wa Netherlands hapa nchini Tanzania. Uzinduzi huo uliongozwa na H.E. Amb. Wiebe de Boer, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania.

Wadau mbalimbali waliohudhulia hafla ya Uzinduzi wa Mradi kutoka Shirika la Global Peace Foundation nchini Tanzania

Mradi huu, utakaotekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja, unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi katika Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, na Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi. Lengo kuu la mradi ni kutatua changamoto zinazozuia jamii kujikita katika ulinzi shirikishi, ikiwemo ukosefu wa juhudi za pamoja kati ya mifumo iliyopo, ukosefu wa ushiriki wa wanawake katika shughuli za ulinzi shirikishi, na mapungufu katika miundombinu ya kiutendaji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mheshimiwa Victoria Mwanziva, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, alisisitiza kuwa mradi huu unalenga kuboresha mbinu na ujuzi wa kiutendaji miongoni mwa maofisa wa Jeshi la Polisi. Aliongeza kuwa pia utaongeza uwelewa wa kanuni, misingi, na manufaa ya ulinzi shirikishi katika jamii, huku ukisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake na vijana katika masuala ya ulinzi na usalama. Aidha, alieleza kuwa mradi huu utaanzisha mifumo ya upashanaji habari na ushirikiano kati ya Polisi Jamii na jamii kwa ujumla.

 

Pichani ni Hussein Sengu ambaye ni Director wa Shirika la Global Peace Foundation nchini Tanzania

Mradi huo utafanikishwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza itahusisha kutambua mahitaji ya jamii, kushirikisha wananchi, na kutengeneza mtaala wa mafunzo. Awamu ya pili itahusisha kufanya majaribio ya mtaala huo, kufanya kampeni za kuongeza uwelewa wa jamii kuhusu ulinzi shirikishi, na kuhamasisha juhudi za pamoja za wanawake katika masuala ya usalama. Mradi huu unalenga kuwafikia wananchi, wanawake, vijana, na vyombo vya ulinzi kutoka mikoa ya Ruvuma na Lindi.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post