Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Musabila Kusaya. Akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) |
TAARIFA KWA UMMA
UKAMATAJI WA KILO 16.643 ZA DAWA ZA KULEVYA
Dar es Salaam, 07 Disemba, 2022
Katika kipindi cha mwishoni mwa mwezi Novemba 2022, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilifanikiwa kukamata jumla ya kilo 16.643 za dawa ya kulevya zikijumuisha kilo 15.19 za heroin, gramu 655.73 za cocaine na gramu 968.67 za Methamphetamine zilizowahusisha jumla ya watuhumiwa saba.
Ukamataji wa kilo 15.19 za dawa za kulevya aina ya heroin zilizowahusisha watuhumiwa watatu ni mwendelezo wa operesheni zilizopita. Watuhumiwa hawa ni washirika wa Kambi Zuberi Seif na wenzake waliokamatwa wakiwa na kilo 34.89 za heroin katika operesheni ya mwanzoni mwa mwezi Novemba 2022.
Watuhumiwa hao watatu ni Suleiman Thabit Ngulangwa (36), mfanyabiashara na mkazi wa Salasala, Sharifa Seleman Bakar (41), mkazi wa Maji matitu - Mbagala na Farid Khamis Said (22) mkazi wa Maji matitu – Mbagala, wote ni wakazi wa Dar es Salaam.
Watuhumiwa wengine wanne (4) walikamatwa wakiwa na gramu 655.75 za cocaine na gramu 968.67 za Methamphetamine. Walikamatwa wakiwa kwenye harakati za kusafirisha dawa hizo za kulevya kwenda nje ya nchi. Watuhumiwa hao wanne ni Hussein Rajab Mtitu (28) anayejulikana pia kama Chodri Mohamed mfanyabiashara na mkazi wa Kibonde maji, Mbagala, Jaalina Rajab Chuma (31) anayejulikana pia kama Jaalina Mohan mjasiriamali na mkazi wa Tandika, Shabani Abdallah Said (36) mkazi wa Kilimahewa, Tandika, hawa pia ni wakazi wa Dar es Salaam, pamoja na Irene Dickson Mseluka (39) mfanyabiashara na mkazi wa Ndala Shinyanga. Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za kiupelelezi kukamilika.
Kutokana na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya nchini, wahalifu wa dawa za kulevya wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali ili kufanikisha uhalifu wao. Hata hivyo, Mamlaka iko macho na inaendelea kukabiliana na mabadiliko ya mbinu hizo. Aidha, tunashirikiana na makampuni ya usafirishaji wa vifurushi, vyombo vyote vya ulinzi na usalama na wadau wengine katika udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kukabiliana na mbinu mpya za usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.