Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 05
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 05 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA....!!! Kila mtu aliangalia maisha yake, kila mtu alitaka kuiokoa ...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 05
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 05
ILIPOISHIA....!!!
Kila mtu aliangalia maisha yake, kila mtu alitaka kuiokoa nafsi yake. Ndani ya sekunde ishrini tu, ndani ya uwanja huo walibaki watu wawili tu. Saida na mwanamke huyo aliyekuwa na mabomu ambaye muda wowote ule alikuwa akilia kuomba msaada.

SASA SONGA NAYO...!!
Kareem alichanganyikiwa, kitendo cha Saida kuhukumiwa kifo kilimuuma moyoni mwake. Hakutaka kuona hilo likitokea, alipanga kufanya mipango kabambe mpaka kuhakikisha mpenzi wake anatoka salama.

Alikuwa amebakiza saa chini ya kumi na nane tu kabla ya mpenzi wake kupigwa mawe na kufa. Hakutaka kuchelewa, usiku huo ambao polisi walimchukua na kuondoka naye, alichokifanya ni kuwasiliana na rafiki yake, mhuni aliyekuwa akiishi mbali na nyumbanii hapo katika Mtaa wa Al Masjidir ambao ulikuwa na wahuni wengi, Jamaa huyo aliitwa Hassan Muntazir.

Kitendo cha kusikia kwamba alikuwa akitafutwa na Kareem, moyo Hassan ukahisi furaha ya ajabu, halikuwa jambo la kawaida kutafutwa na mtoto wa kishua kama yeye, alijua kwamba ni lazima kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kukataa, wakapanga sehemu na kuonana huko.

Wakakutana katika mgahawa mmoja na kuzungumza, Kareem hakutaka kumficha Hassan, alimwambia ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea na kwamba alihitaji msaada wake wa nguvu na mali.

“Nikusaidie nini katika hili? Mbona naona kuna ugumu sana?” aliuliza Hassan, alikuwa akimwangalia Kareem huku kichwa chake kikiwa na maswali mengi.

“Hakuna ugumu Hassan!”
“Kivipi? Tufanye nini unavyoona?”
Hapo ndipo Kareem alipoanza kumwambia mpango wake kwamba ilikuwa ni lazima waondoke na kuelekea katika uwanja wa mauaji kwa ajili ya kuchukua mawe yaliyokuwa ndani ya uwanja huo.

Hilo halikuwa kazi kabisa, uwanjani hapo hakukuwa na mlinzi, hawakuwahi kufikiria kwamba kungetokea na mtu ambaye angefika huko na kuiba mawe. Hilo likaonekana kuwa jambo jepesi. Kareem akamwambia Hassan kwamba alitakiwa kuondoka na kuwaita marafiki zake ili wasaidiane katika hilo.

“Mmh! Ngoja tujaribu!”
“Haina shida. Waambie waje na gari kubwa ili tubebe yale mawe. Ngoja nikamtafute mtu wa ufunguo,” alisema Kareem.
Hilo ndilo alilolifanya. Kitu cha kwanza kilikuwa ni kwenda katika uwanja huo kwa ajili ya kuipiga picha kufuli ili awapelekee wataalamu wa kuchonga funguo waweze kufanya kazi hiyo.

Hilo halikuwa tatizo, akaelekea huko, hakukuwa na walinzi hivyo alichokifanya ni kulipiga picha kufuli na kisha kuondoka zake. Hakutaka kurudi nyumbani, akaanza kuwasiliana na wachonga funguo ambao kwa kipindi hicho walikuwa wamelala lakini kwa sababu waliahidiwa fedha nyingi, wakakubaliana naye.

Funguo zikaanza kuchongwa, haikuwa kazi kubwa, kutokana na umahili wao wa uchongaji, walitumia nusu saa tu wakawa wamefanikiwa na kumkabidhi funguo zake mbili na kuondoka.

“Hassan! Umefikia wapi?” aliuliza Kareem kwenye simu. Tayari ilikuwa saa sita usiku.
“Ndiyo tumemaliza kuelewana na mwenye gari, amesema poa,” alisikika Hassan kutoka upande wa pili.
“Safi sana. Amesema anataka kiasi gani?”
“Anata rial elfu moja!”
“Hakuna tatizo! Mwambie nitampa. Chukueni gari kwanza, halafu asijue mnakwenda wapi,” alisema Kareem.

“Sawa mkuu! Kwa hiyo tukutanie wapi?”
“Uwanjani! Ila mkianza kuingia maeneo hayo, zimeni taa kabisa ili kusiwe na yeyote atakayewaona,” alisema Kareem.
Hilo halikuwa tatizo kabisa. Hassani na wenzake wakafanya kama walivyoambiwa. Wakachukua gari na kuelekea katika uwanja wa kifo. Walipokaribia kufika huko, taa zikazimwa na gari kuanza kwenda pasipo taa.

Walipofika, Kareem akafungua kufuli na kisha kuingia ndani. Huko, kama walivyopanga ndivyo walivyofanya, wakaanza kupandisha mawe kutoka ndani ya uwanja huo mpaka garini.

Ilikuwa kazi kubwa na nzito iliyowachukua saa moja na nusu mpaka kumaliza. Baada ya hapo, wakaondoka huku wakiwa wamesahau kama ndani ya uwanja ule, mbali na mawe kulikuwa na fimbo.

“Tumefanikiwa! Nashukuru sana,” alisema Kareem, akawalipa watu hao kiasi cha fedha walichokihitaji na mawe kwenda kutupwa sehemu.

Kazi kubwa alikuwa ameimaliza lakini bado mbele yake kulikuwa na safari kubwa. Alijua kwamba mpenzi wake angefikishwa ndani ya uwanja huo hivyo ilikuwa ni lazima awapange watu wengine.

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtafuta mtengeneza mabomu. Alimwambia kwamba alitaka kutengenezewa bomu la bandia ambalo angekwenda kulitumia sehemu, hiyo nayo haikuwa tatizo. Alikuwa na fedha na kila alipokwenda fedha ilitumika.

Kwa sababu lilikuwa bomu bandia, hakukuwa na kazi kubwa ya kutengenezewa, baada ya saa moja, akapewa na kurudi zake nyumbani huku ikiwa ni saa nane usiku.

Hakutaka kulala hata mara moja, ilikuwa ni lazima ahakikishe kila kitu kinafanyika usikui huohuo. Alichokifanya ni kuwasiliana tena na Hassan na kumwambia kwamba kazi haikuwa imekwisha bali alichokitaka ni kuandaliwa mwanamke.

“Wa nini tena?”
“Kwanza upo wapi?”
“Kijiweni na washikaji!”
“Nakuja!”
“Usiku huu?”
“Kwa tatizo nililokuwa nalo! Huu ni mchana! Naomba uniandalie mwanamke,” alisema Kareem.

“Hakuna tatzio! Kuna Yasmin hapa!”
“Huyoohuyo atafaa.”
Hiyo ilikuwa ni kazi ya usiku kwa usiku, hakukuwa na muda wa kupumzika, japokuwa alikuwa amezunguka sana lakini hakuchoka. Akamfuata Hassan na kumwambia lengo lake, msichana huyo alikuwa mahali hapo hivyo alitakiwa kupewa mchongo mzima utakavyokuwa.

“Hakuna tatizo! Si umesema bomu la bandia?” aliuliza Yasmin.
“Ndiyo!”
“Basi hakuna tatizo!”
“Ila nitataka unisaidie kitu kimoja.”
“Kipi?”
“Vaa majuba mawili, moja liwe lako na jingine la yule msichana. Uwe na nikabu kwa ajili ya msichana yule, yaani kila kitu uwe navyo viwiliviwili. Ukifika na kufanikiwa, watu wakikimbia, mwambie avae nguo nyingine ulizokuja nazo na mtoke nje. Mkifika, Hassan na wenzake wakakuwa wakiwasubiri kwenye gari jingine hapo nje,” alisema Kareem.

“Na kama atakuwa amefukiwa, nitaweza kufukua shimo kwa haraka?” aliuliza Yasmin.
“Atakuwa hajafukiwa. Hakuna mawe huko, hivyo hilo usijali,” alisema Kareem.
“Mmh!”
“Naamini utaweza!”
“Sawa. Nitafanya hivyo!”

Mpaka ilipofika asubuhi, kila kitu kilikuwa kimeandaliwa. Harakaharaka mipango ikakamilika, gari likatafutwa na muda ambao polisi walikuwa wakiondoka na Saida kwenda kule kwenye uwanja wa kifo, nao walikuwa nyuma wakifuatilia.

“Tukae hapahapa,” alisema Hassan na kusimama nje ya uwanja ule huku ndani ya gari hilo wakiwa watatu tu.
Walikaa hapo kwa dakika kadhaa ndipo wakaanza kusikia kelele kutoka ndani ya uwanja huo, watu wakaanza kutoka huku wengine wakiruka ukuta. Tayari wakajua kwamba Yasmin alifanya kile walichotaka kukifanya.

Ndani ya uwanja huo, Yasmin alijifanya akilia, Saida alibaki akitetemeka, msichana aliyekuwa mbele yake alikuwa na mabomu ya kujitoa mhanga aliyokuwa ameyavaa mwilini mwake. Alitetemeka, hakujua ni kitu ganii alitakiwa kufanya.

“Don’t run, I am here to help you!” (usikimbie! Nipo hapa kukusaidia) alisema Yasmin.
“To help me or kill me?” (kunisaidia au kuniua?)
“To help you! Put those on.” (Kukusaidia. Vaa hizi)

Akampa nguo zile, juba, nikabu na kumwambia kwamba alitakiwa kuvaa harakaharaka. Yasmin alibaki akishangaa, hakumfahamu msichana huyo wa Kiarabu alitoka wapi lakini kwa sababu alimwambia kwamba alikuwa hapo kwa lengo la kumsaidia, akavaa harakaharaka na kutoka nje.

Hakukuwa na mtu, watu wote wakiwemo polisi walikuwa wamekimbia. Walipotoka nje ya geti tu, harakaharaka Hassan na wenzake wakawafuata na kuwaambia waingie ndani ya gari. Wakaingia na kuanza kuondoka.

“Who are you?” (nyie ni wakina nani?)
“Kareem’s friends...do you know him?” (marafiki zake Kareem....unamfahamu?)
“Yes!”
“He is the one who sent us!” (ndioye aliyetutuma) alijibu Hassan huku Hussein, rafiki yake akifanya kazi ya kubadilisha gia tu.

Je, nini kitaendelea? USIKOSE SAA MOJA JIONI

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top