"ukosefu
wa ajira kwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka."
Kauli
hiyo siyo ngeni masikioni mwetu,tumekuwa tunaisikia mara kwa mara. Bila shaka
wanaosema hivyo wamefanya utafiti na kugundua athari za vijana kutokuwa na
ajira.
Haijalishi kama baadhi ya wanaosema hivyo kwa maslahi yao ya kisiasa kwa
kutumia tatizo la ajira kwa vijana kama mtaji na daraja la kufikia malengo yao
kisiasa badala ya uchungu unaotokana na kubaini madhara yanayoweza kutokea kwa
kukosekana mipango na usimamizi kamambe wa kulijali kundi hilo kubwa la
kijamii.
Lakini
bado shaka waliyonayo ni yakweli na utabiri wao unaweza kutimia iwapo
hazitachukuliwa hatua za haraka na madhubuti ya kuzuia hali hiyo ambayo binafsi
siombei itokee. Niukweli usiopingika kwamba serikali imekuwa na mikakati na
mipango kamambe ya kuwafanya vijana waweze kujiajiri.
Serikali
kwa kutambua umuhimu na changa moto zinazozikabili kundi hili na wanawake
imezitaka halmashauri kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili
ya mifuko ya vijana na wanawake.
Pamoja na
sheria kuzitaka halmashauri kufanya hivyo lakini ni kama kuna mgomo baridi
katika utekelezaji. Maana halmashauri nyingi hazitengi na kupeleka fedha kwenye
mifuko hiyo kwa uwiano wa mapato yake ya ndani na kwa wakati.
Maana
yake nikwamba mpango mkakati huo unabaki ni wakufikirika kama ilivyo kwa
mipango mkakati na sera nyingine ambazo zinafanana na uzuri wa makaburi ambayo
yamejengwa na kupambwa kwa marumaru lakini kilichomo ndani hakina uhai na
kimeoza.
Kinachosababisha
hali hiyo ni kukosekana kwa usimamizi madhubuti wa mipango na sera, ambazo
zipo kwenye vitabu vilivyofungiwa makabatini na vishubaka. Hata hivyo wapo
viongozi wachache miongoni mwa wengi ambao naamini wameliona tatizo lililopo na
madhara yanayoweza kutokea iwapo uzembe katika kuzuia utaendelea.
Miongoni
mwa hao wachache ambao wamebaini ukweli huo na kuanza kuchukua hatua kwa
vitendo ni mkuu wa mkoa wa Lindi, Mwantumu Mahiza. Mkuu wa mkoa huyu miongoni mwa
wakuu wa mikoa wachache wanawake, ambaye kama kumbukumbu zangu kama zipo sawa
hajachukua hata miezi minne tangu ahamishiwe katika mkoa huu kutoka mkoa wa
Pwani ameamua kufanya ambalo wengi walishindwa kufanya na bado wanashindwa
kufanya iwe kwa uzembe, kutojua wajibu wao au kutojua madhara yanayoweza kutokea
kutokana na kushindwa kuchukua hatua.'Eria kamishina (jina la kabla ya uhuru)
huyu ambaye kwa sasa anaitwa rejino kamishina (mkuu wa mkoa) katika ziara zake
za kujitambulisha, kutembelea na kukagua shuguli mbalimbali za maendeleo
katika wilaya za mkoa wa Lindi. Pamoja na mambo mengine alikuwa anasisitiza
umuhimu wa halmashauri za manispaa, miji na wilaya zilizopo katika mkoa huu
kutekeleza kwa vitendo agizo (sheria) ya kupeleka asilimia kumi ya mapato yake
ya ndani kwenye mifuko ya vijana na wanawake na asilimia 60 zipelekwe kwenye
miradi ya maendeleo.
Hiyo
ilitokana na kutoridhishwa na utekelezaji wa sheria hiyo uliofanywa na
halmashauri, ambazo ziliamua kutumia fedha hizo kwa shughuli nyingine au
kukosekana kwa maelezo ikiwemo kuongezea katika Ujenzi wa Maabara kutekeleza
Agizo Rais.
Katika
kuonesha kuwa alikuwa hatanii (hakuwa na masihara) katika hilo alihaidi kuwaita
vijana kutoka kila wilaya za mkoa huu ili wapewe mafunzo yatakayowazesha
kuzitambua na namna ya kuzitumia fursa zilizo katika maeneo yao ili waweze
kujiari na kujiletea maendeleo.
Huku
akiwaagiza viongozi na watendaji kuwateua vijana bila ya upendeleo na itikadi
za siasa, imani za kidini na ukabila wao. Binafsi niliamini alikuwa
anafanya siasa (porojo) kama ilivyozoeleka Kwa viongozi wetu walivyojaaliwa
kuipepeta midomo yao na kuwapa wananchi matumaini yenye uzito mithili ya
maputo.
Kumbe
kama wenye busara zao wanavyotuasa kwamba mazoea siyo sheria na mtu haukumiwi
kwa histora bali matendo ya wakati kwa makosa na mema ya wakati husika.
Mimi ni miongoni
mwa wachache niliyekuwa naamini katika historia na mazoea katika kutoa hukumu. Nakiri
kuwa nilifanya kosa kuamini hivyo Kwani Mkuu huyu wa mkoa alitimiza aliloliahidi
kwa kufanikiwa kuwakusanya vijana 360 kutoka katika halmashauri sita za
mkoa huo. Ambapo walipata mafunzo kwa muda wa siku tano, kuanzia tarehe 23 hadi
27 Februari mwaka huu.
Vijana
hao walipewa mafunzo ya ujasiriamali ikiwamo kutumia fursa zilipo katika maeneo
yao, faida za kujiunga na mifuko ya kijamii, mifuko ya afya na namna ya kupambana
na rushwa Ambapo wataalam bobezi wa
masuala hayo walitoa mada na hatimaye kufanya mijadala ya kina kuhusiana na
mada husika zilizowasilishwa.
Kupitia
semina hiyo baadhi ya Taasisi zimehaidi kusaidia mitaji na mikopo kwa vijana
hao ambao ni mabalozi wazuri kwa wenzao ambao hawakushiriki semina hiyo.
Kwangu
mimi kitendo hiki kilichofanywa na Mahiza ni cha kupongezwa na kupigiwa mfano Bila
shaka kama viongozi na watendaji wetu watakuwa na mwenendo kama huu, tunaweza
kufika pale ambapo wenzetu wamefika kimaendeleo na kuepuka tishio na kauli za
kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ambao ni bomu linalosubiri kulipuka.
Nimalize
makala yangu kwa kuomba vijana waliopata mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri
watakao fikisha maarifa waliyopata kwa wenzao, wakati wakiyafanyia kazi kwa
vitendo mafunzo hayo hasa baada ya kuwezeshwa mitaji na vifaa kama
walivyohaidiwa.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.