Unknown Unknown Author
Title: WAZIRI WA NISHATI NA MADINI AFANYA ZIARA YA KIKAZI MIKOA YA LINDI NA MTWARA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Sehemu ya Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba – Mtwara. Na Veronica Simba Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amefa...
Msimbati
Sehemu ya Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba – Mtwara.

Na Veronica Simba
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amefanya ziara mkoani Lindi na Mtwara mwanzoni mwa wiki kukagua miradi mbalimbali iliyo chini ya Wizara yake ambapo aliahidi huduma za umeme na maji kwa wananchi mbalimbali.

Akiwa Madimba mkoani Mtwara, baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi, Waziri Simbachawene alimwagiza Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Bomba la gesi, Mhandisi Kapuulya Musomba kutoa huduma ya maji safi kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

“Kutokana na taarifa yenu, mtakuwa na hifadhi ya maji ya kutosha hapa. Pamoja na matumizi yenu mbalimbali, hakikisheni mnatoa huduma ya maji kwa wananchi wanaozunguka mtambo,” alisema Waziri. Vilevile, Waziri Simbachawene alitoa ahadi ya umeme kwa Kijiji cha Luvula kilichoko Msimbati. Alisema Kijiji hicho na vingine 15 vilivyo jirani na Kiwanda cha kufua umeme cha Mnazibay, vitapatiwa umeme kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu.

“Tunaendelea na zoezi la kusambaza umeme nchi nzima. Lengo letu ni kuhakikisha idadi ya watanzania wanaopata umeme inaongezeka zaidi na zaidi ili kuwezesha lengo la nchi yetu kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama dira ya maendeleo inavyoonesha,” alisema.

Ziara hiyo ya Waziri Simbachawene, ni ya kwanza kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara tangu aliposhika wadhifa wa Uwaziri wa Nishati na Madini, Januari mwaka huu.


Msimbati
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda (aliyesimama), akiwasilisha taarifa fupi ya hali ya mmomonyoko wa ardhi uliosababisha mazingira ya hatari kwa Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Maurel & Prom Tanzania (M&P), kilichopo Mnazi Bay – Mtwara. Wanaosikiliza ni Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (wa tatu kutoka Kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu (katikati), na baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini walioongozana na Waziri.
Msimbati
Meneja Uzalishaji na Uendeshaji wa Kampuni ya Maurel & Prom, David Chajdronnier (katikati) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (Kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Hawa Dendegu (Kulia) kuhusu mmomonyoko wa ardhi eneo la MnaziBay, Mtwara. Kampuni hiyo ndiyo inazalisha umeme unaotumiwa na wakazi wa Mtwara na Lindi.
Msimbati
Mwenyekiti wa Kijiji cha Luvula, Msimbati mkoani Mtwara, Yusuf Haki Yusuf (Kulia) akiwasilisha maombi ya wananchi wa Kijiji chake kupatiwa umeme kwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (wa pili kushoto) wakati wa ziara yake mwanzoni mwa wiki. Waziri aliahidi kuwa Kijiji hicho na vingine 15 vilivyo jirani na MnaziBay vitapatiwa umeme kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu. Kulia kwa Waziri, ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu.
Msimbati
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, (aliyenyoosha mkono) akimwonyesha kitu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu (wa pili kulia) wakati Waziri alipotembelea eneo hilo kujionea athari za mmomonyoko wa ardhi uliotishia usalama wa mazingira ya Kampuni ya kufua umeme ya Maurel & Prom iliyo jirani na eneo hilo.
Msimbati
Athari ya mmomonyoko wa ardhi katika eneo la MnaziBay inavyoonekana pichani. Mmomonyoko huo umetishia usalama wa Kiwanda cha kufua umeme unaotumiwa na wakazi wa Lindi na Mtwara cha Maurel & Prom.
Msimbati
Baadhi ya nyumba wanazoishi wafanyakazi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba – Mtwara.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha ziara yake kukagua Mtambo wa kuchakata gesi wa Madimba – Mtwara. Kulia kwa Waziri ni Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, Mhandisi Kapuulya Musomba na kushoto kwa Waziri ni Mkuu wa Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top