Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI "NIMEPATA NJIA SEHEMU YA PILI"
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
ILIPOISHIA "Dada kwanini baba amekuwa hivyo, inamaana hawezi tena kuongea, dada Baba aliniambia atanipeleka shule, inamaana hanipe...


ILIPOISHIA
"Dada kwanini baba amekuwa hivyo, inamaana hawezi tena kuongea, dada Baba aliniambia atanipeleka shule, inamaana hanipeleki tena, kwanini Baba yangu anatoka damu, halafu wanambeba na kumuweka kwenye gari, dada mimi namtaka Baba yangu". Aliongea Rony kwa uchungu sana dada yake alishindwa kumjibu chochote alimkumbatia na kuendelea kulia kwa uchungu.

INAPOENDELEA
Ritha alikuwa ni msichana mdogo ambapo kwa wakati huo alikuwa kidato cha tatu, na alikuwa na wadogo zake wawili mapacha ambaye ni Rony na mwingine anaitwa Rosada. Siku zote walikuwa wakiishi na Baba yao kwani Mama yao mzazi aliwaacha Rony na Rosada wakiwa wadogo sana kipindi Mama Ritha anaondoka walikuwa na miezi tisa, wakati Ritha alikuwa anasoma darasa la nne.

Mzee Jengo alikuwa ni mfanyabiashara wa vifaa vya kilimo na mkulima, ambapo kwa namna moja au nyingine alikuwa ni Mzee mwenye uwezo kifedha, siku zote za maisha yake alikuwa ni mchapa kazi, alijituma sana katika kufanya kazi kwa bidii na ndiyo maana aliweza kufanikiwa na kuwa na maisha mazuri. Alikuwa anafahamika na watu wengi kwasababu alikuwa akiishi na watu vizuri na aliwasaidia watu mbalimbali wakiwemo ndugu jamaa na marafiki na hata wale asiowafahamu. Alikuwa ni mcheshi na mkarimu sana.

Hivyo taarifa za kifo chake ambacho kilitokea ghafla kiliwashtua watu wengi sana, ambao walikusanyika katika kuomboleza kwenye nyumba ya Mzee Jengo. Simanzi na vilio viliendelea kutawala akina Mama na akina Baba na watoto walilia kwa uchungu sana, taratibu za mazishi ziliendelea baada ya ndugu wa Marehemu kufika na siku ya kumpumzisha Mzee Jengo katika makazi yake ya milele ilifika. Siku hiyo Ritha alikuwa kimya asiyeongea chochote ila alionekana kuwa mwenye mawazo mengi sana na alikuwa amechoka kutokana na kupoteza fahamu mara kwa mara.

Rony na Rosada walikuwa wameketi na shangazi yao anayeitwa Mama Sara ambaye alikuwa akiwabembeleza wasilie. Ulifika muda wa kwenda kumuaga marehemu kwa mara ya mwisho ambapo walianza ndugu wa marehemu na baadaye watoto wa marehemu. Ritha alipofika karibu na Jeneza alisimama na kumshika Baba yake kwenye paji la uso huku akilia kwa uchungu “Baba, baba amka baba embu tizama sisi tutabaki na nani, Baba amka Baba inamaana kweli huwezi kuongea jamani Baba yangu uwiiiiii jamani Baba yangu uwiiii Baba ulisema nikifaulu utaninulia zawadi sasa mbona umeondoka baba”.
Ritha alikuwa akiongea kwa uchungu huku machozi yakiendelea kumbubujika, shangazi yake alimshika na kumsogeza pembeni huku akiendelea kumfariji “Mwanzangu Ritha nyamaza usilie, haya yote ni mapenzi ya Mungu, Baba amepumzika mahali pema peponi, tafadhali nakuomba ujikaze mwanangu” Alimfariji Mama Sara lakini Ritha aliendelea kulia bila ya kupumzika na wakati huo Rony alipofika kumuona Baba yake kwa mara ya mwisho masikini aliishiwa nguvu na kuanguka chini.

Ndugu walimbeba na kumlaza pembeni huku wakimpatia huduma ya kwanza, kwa upande wa Rosada alipomuona Baba yake akiwa amelala usingizi wa milele alianza kulia huku akisema “Mtoeni Baba yangu, kwanini mmemuweka huku, Baba amka, Baba amka jamani mtoeni Baba yangu namtaka Baba yangu” Aliongea Rosada huku akilia sana.

Watu wengi walilia sana kwa namna wavyokuwa wakiwatizama wale watoto walivyokuwa wakilia na kuongea kwa uchungu. Mmoja kati ya waliohuduria msibani alisikika akisema “Jamani hawa watoto wanasikitisha sana, embu tizama wanavyolia, na Baba yao alikuwa akiwalea peke yake, yaani Mama yao sijui yuko wapi, halafu yule Mama ni mjinga sana inamaana hata taarifa za msiba hajazipata au inakuwaje inaumiza sana kwakweli”.
Alizungumza dada mmoja huku akimgeukia rafiki yake ambaye walikuwa wamekaa pamoja, na kuendelea kunong’ona “Mwenzangu yaani Mama yao sijui ni mtu wa namna gani anawezaje kuwaacha watoto wanaishi na Baba yao pekee, yaani hawa watoto hawajui mapenzi ya Mama kabisa kwani aliwaacha wadogo sana, ila huyu Baba Mungu ampunzishe mahali pema peponi jamani amehangaika sana na hawa watoto” Aliongea yule dada ambaye alionekana kuifahamu vizuri familia ya Mzee Jengo.

Taratibu ziliendelea na hatimaye Mzee Jengo alipumzika katika makazi yake ya milele na huo ndiyo ukawa mwisho wa maisha ya Baba Ritha. Maisha yaliendelea huku familia ikiwa imebaki na simanzi kubwa na baada ya matanga, watoto waliendelea kuishi na Baba yao mdogo ambaye alikuwa anaitwa Ndama.

Hali ya maisha ilibadilika kwa upande wa Ritha kwani muda mwingi alikuwa akionekana kuwa mwenye mawazo mengi sana, siku moja alikuwa ameketi chumbani kwake huku akiwa anawaza “Baba umetuacha peke yetu, yaani sisi ni kama yatima, ijapokuwa tunaishi na Baba mdogo, lakini ni tofauti na tulivyokuwa tunaishi na wewe, hata kama Baba mdogo anatuonyesha upendo wa dhati lakini kamwe pengo lako halizibiki Baba, natamani ungekuwepo.

Aliwaza Ritha huku akiendelea kulia na kutafakari "Nikifikiria Mama alituacha tukiwa wadogo, tena bila hata ya huruma, na hata sijui yuko wapi, angalau Mama angekuwa anatupenda, tungepata faraja lakini ametutupa na kutuacha peke yetu wakati mwingine huwa najiuliza hivi kweli ni Mama yangu mzazi? Kwani nikitizama marafiki zangu wanavyopata mapenzi ya dhati kutoka kwa Mama zao, siamini kama Mama yetu alitutekeleza, eeh Mungu naomba utusaidie, Moyo wangu unaumia sana, najiona kama nina kidonda ambacho hakiwezi kupona hata nikipewa dawa yoyote ile.” Alikuwa akiwaza Ritha huku machozi yakimtoka.

JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA TATU ITAENDELEA SIKU YA JUMANNE.

KWAHISANI YA ADELA KAVISHE BLOG

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top