Unknown Unknown Author
Title: PROFESA LIPUMBA AWASHA MOTO WILAYANI NACHINGWEA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelaani kitendo cha amriya Serikali kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadha...

lipumbaMWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelaani kitendo cha amriya Serikali kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Profesa Lipumba, alitoa lawama hizo kwa Serikali juzi, wakati alipokuwa akimnadi mgombea udiwani, Hamisi Malibiche, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Kata ya Namikango wilayani Nachingwea.

Katika hotuba yake, Profesa Lipumba alisema, amri hiyo ya Serikali ina sura ya kibaguzi, hasa kutokana na sababu zinazoelezwa na Serikali za kuzuia mikutano kukosa mashiko.

Profesa Lipumba, alihoji kama sababu ni maandamano na fujo zilizotokana na wananchi wa mikoa hiyo, imekuwaje hadi sasa amri hiyo iendelee kuzingatiwa hali ya kuwa hakuna vurugu.

“Amri hii ni ya kibaguzi, kwani sababu inayoelezwa na Serikali kuwa imezuia kwa sababu za kiusalama, haina nguvu tatizo hapa ni kutokana na wananchi kuhoji maendeleo yao siyo suala la usalama.

“Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010, Rais Jakaya Kikwete alinadi ilani ya uchaguzi ya CCM akisema, Serikali itajenga kiwanda cha kufua umeme.

“Pia Rais Kikwete, alitoa taarifa ya kuwa na mradi mkubwa wa umeme baada ya kufika 2013, ikahamia kwenye ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, hivi kuuliza ahadi zisizotekelezwa ni kosa kiasi cha kuzuia mikutano ya vyama vya siasa”? alihoji.

Profesa Lipumba alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa, Serikali ilitenga Sh bilioni 680 kwa ajili ya mradi mkubwa wa kufua umeme, lakini fedha hizo hazijulikani zilikokwenda na matumizi yake pia hayafahamiki.

“Wameshindwa kutimiza ahadi, sasa Serikali inawachonganisha wananchi wa mikoa ya kusini wanataka watumie rasilimali za nchi peke yao,” alisema.

Mwenyekiti huyo pia alitoa shutuma kwa Serikali, kuendelea kulazimisha mfumo wa stakabadhi ghalani kutumika katika ununuzi wa zao la korosho wakati mfumo huo unapingwa na wananchi.

Alisema mfumo huo hauwezi kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri ya zao hilo, kwani hakuna ushindani katika ununuzi ambao ungesababisha kupandisha thamani ya zao hilo.

Lipumba alishauri mfumo huo ufutwe na zao hilo linunuliwe kwa mtindo wa soko huria, ili wafanyabiashara washindane katika kununua kama ilivyo kwa zao la ufuta.

Alisema kuwa, Serikali hali hiyo ni kuendelea kuwakandamiza wananchi wa mikoa ya kusini, wakati wananchi wa mikoa mingine mazao yao hayanunuliwi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

“Ndugu zangu Tabora wanazalisha Tumbaku, Moshi wanazalisha Kahawa, Bukoba wanazalisha Kahawa, lakini hawauzi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, sasa kwanini wananchi wa mikoa ya kusini mnyanyaswe kwa mfumo wa stakabadhi ghalani?” alihoji.

Chanzo - Mtanzania

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top