MACHAFUKO yanayoendelea ndani ya Baraza la Mawaziri, ni wazi yanawaweka waheshimiwa wengi katika wakati mgumu ambapo Jumapili iliyopita, Uwazi lilimnasa mmoja wa mawaziri (jina tunalo), kwenye nyumba ya sangoma aliyefahamika kwa jina moja la Bwehe, Kijiji cha Mlingotini, Bagamoyo, Pwani.
Habari zinadai waziri huyo alikwenda kwa Bwehe ili kufanyiwa madongoloji (nguvu za giza), lengo kuu likiwa kuimarisha nyota yake ili Rais Jakaya Kikwete atakapofanya pangua pangua, jina lake liendelee kutamalaki.
Awali, Jumamosi iliyopita Uwazi lilipokea simu kutoka kwa msomaji wetu aliyesema: “Uwazi kama kweli nyie ni gazeti la kufichua maovu, fikeni Mlingotini kesho asubuhi mtamuona mheshimiwa … (anataja jina la waziri) kwa mganga wa kienyeji.”
Timu ya gazeti hili ilianza safari alfajiri ya Jumapili iliyopita na ilipotimia saa 12:50, tayari ilikuwa imekwishawasili Mlingotini na kupiga kambi jirani na kwa Bwehe.
Hata hivyo, ugunduzi wa waandishi wetu ni kwamba wengi waliosema hawakumuona, ni dhahiri hawamjui, kwa hiyo haikuwa rahisi kupata taarifa zake.
Saa 3:35 asubuhi, waziri huyo alikuwa hajawasili, hivyo kuanza kuzitilia shaka taarifa za mtoa habari.
Timu ya Uwazi, ilituma taarifa makao makuu kwamba taarifa za waziri huyo inaonekana ni feki lakini muongozo wa kuendelea kusubiri ulifanikisha jawabu ilipotimia 3:54, pale gari aina ya Nissan X-trail lilipowasili nyumbani kwa sangoma huyo.
Kilichotendeka ndani hakikuweza kujulikana lakini waziri huyo alitumia takriban saa 4, kwani saa 8:07 mchana alitoka, akaingia kwenye gari na kutoweka.
Jitihada za waandishi wetu kumuwahi ili kumuhoji sababu ya kwenda kwa sangoma ilishindikana maana alipiga hatua kama za umeme kutoka ndani, kuingia kwenye gari, kuwasha na kuondoka.
Mwandishi wetu alipomtafuta waziri huyo kwa simu, alipopatikana na kuulizwa ni kwa nini alikwenda kwa sangoma, alinyamaza kwa sekunde kadhaa kisha akazima simu.
Bwehe alipoulizwa na mwandishi kuhusu mgeni wake ambaye ni waziri, alikuwa mkali, akasema: “Mnataka kuingilia kazi yangu? Mnataka kujua nguvu nilizonazo? Endeleeni kunifuatilia na mtaniona.”
Habari zinasema kuwa tangu machafuko katika Baraza la Mawaziri yatokee, hali imekuwa tete na wengi wao wanaoamini nguvu za giza wamekuwa wakijielekeza kwa waganga wa kienyeji kwa imani kwamba huko ndipo watapata nusura.
Imebainishwa kuwa wimbi la mawaziri kwenda kwa waganga, lilianza tangu Katibu Mkuu wa CCM, Abrahman Kinana, alipozindua kampeni inayoitwa ‘safisha mawaziri mizigo’, hivyo wengi wao kukimbilia kwa sangoma kwa imani kwamba watawezeshwa kukaa upande salama.
Bila shaka, machafuko ya Ijumaa iliyopita bungeni, yaliyofuata baada ya kusomwa kwa ripoti ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, iliyoelezea athari za Operesheni Tokomeza Ujangili (Otu), yanachagiza wenye imani dhaifu kujikita kwa waganga wakiwaona ni wakombozi wao.
Ripoti hiyo, ilisababisha mawaziri wanne, Dk. Hamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Mathayo David (Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo) kung’oka, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa katika kikaango kikali.
Habari zinasema kuwa wakuu wa mikoa kwa nafasi zao za kuwa wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao, wapo kwenye tetemeko kwa sababu unyama waliofanyiwa wananchi, nao hawawezi kupona kwa sababu kama wangewajibika ipasavyo, ukatili uliotendeka usingefanyika.
via GPL
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.