MKAPA NA KASHFA MPYA, SOMA ZAIDI HAPA
MBUNGE wa Nanyumbu, Dustan Mkapa (CCM), anatuhumiwa kujihusisha na biashara ya uvunaji haramu wa mbao na magogo katika msitu wa hifadhi ya Mtambaswala uliopo mkoani Mtwara. Aidha amedaiwa kuorodhesha majina ya uongo ya watu wanaojihusisha na ujangili, ili kufanikisha nia yake ya kukwepa operesheni ya safisha ujangili inayoendeshwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori.
Imedaiwa kuwa hatua ya mbunge huyo imesababisha wananchi wa jimbo lake, kuyakimbia makazi yao kutokana na kuhofia kukamatwa.
Hofu hiyo imekuja kutokana na wanajeshi wanaoshiriki kwenye operesheni hiyo kupiga, kujeruhi na kufikia hatua ya kuua watu wawili.
Wakizungumza na RAI Jumatano kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotajwa majina kwa kuhofia kipigo kinachoendelea kutolewa jimboni humo, baadhi ya wakazi wanaoishi kwenye jimbo hilo walisema kuwa wamehuzunishwa na kitendo cha mbunge wao kuwahusisha na uharibifu wa misitu ya hifadhi.
Mmoja wa wananchi hao, alisema taarifa kuhusu majina yaliyoorodheshwa na mbunge huyo, zilitolewa na mmoja wa askari waliopo katika jimbo hilo.
“Tumeshindwa kumwelewa mbunge wetu, anatambua kabisa kwamba yeye anajihusisha na biashara hii ya kuvuna mbao na magogo kwenye hizo hifadhi kwa kuwatumia baadhi ya vijana hapa vijijini, lakini anatusingizia sisi.
“Anapotugeuka na kudai kuwa sisi ndio tunaohusika na biashara hiyo, tunashindwa kumuelewa kwa sababu hili ni jambo ambalo limeleta madhara kwetu ambao hatuhusiki,” alisema.
Akizungumza na RAI Jumatano, Diwani wa Kata ya Napacho katika Jimbo la Nanyumbu, Mary Mtopa (CCM), alikiri uwepo wa vipigo na vifo katika kata yake, ambavyo vimetokana na operesheni hiyo.
Akizungumzia kuhusu taarifa za mbunge huyo kujihusisha na biashara hiyo, Mtopa alisema hana uhakika kwa kuwa hiyo ni biashara ya siri ambayo huwezi kumfahamu mhusika mara moja.
“Kusema kweli katika kata yangu hali si shwari, wananchi wameyakimbia makazi yao kutokana na operesheni hiyo, ni kweli nimesikia kuna majina wamepatiwa askari, lakini pia sijajua wamepatiwa na nani kwa sababu hili ni suala la kiusalama zaidi.
“Kuna mwananchi mmoja ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya msingi, namfahamu kwa jina moja la Guto, sasa ni marehemu, inasemekana wiki iliyopita alichukuliwa nyumbani kwake usiku yeye na watoto wake wakapelekwa kwenye kambi ya hao wanajeshi inayofahamika kwa jina la Mtema Upinde.
“Walipofika huko kambini kwa mujibu wa maelezo ya watoto wake, wao walirudishwa, lakini siku iliyofuata walipewa taarifa kuwa baba yao yupo hospitali, kumbe alikuwa ameshafariki kwa kipigo alichopewa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Festo Kiswaga, alisema hana taarifa hizo kwa sababu yuko nje ya eneo lake la kazi.
Alipoulizwa Mkapa na RAI Jumatano kuhusu ukweli wa madai hayo, alikana kuhusika na biashara hiyo na hata kuorodhesha majina ya watuhumiwa wa ujangili.
“Si kweli kwamba najihusisha na biashara hiyo, hizo ni propaganda tu zinaendeshwa ndani ya jimbo langu, kwanza nilikuwa naumwa hivyo sifahamu nini kinachoendelea huko,” alisema.
Alipotafutwa Msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba, kuzungumzia madai ya wanajeshi kupiga na kuua raia, alisema kuwa hana taarifa hizo na hata hiyo operesheni ya kusaka majangili haijui.
“Ninachofahamu ni kwamba wanafanya Operesheni Kimbunga na si ya ujangili, ngoja nifuatilie,” alisema.
Madai ya Mkapa kuhusishwa na biashara hiyo yanawiana na yale yaliyowahi kutolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, kwamba wapo baadhi ya viongozi wa Serikali wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
SOURCE: MWANANCHI
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.