Diwani wa kata Nandagala,Andrew Chikongwe akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, mkoa wa Lindi liliokutana siku ya ijuma kwenye ukumbi wa Rutesco.
Ruangwa,Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa,mkoa wa Lindi wametoa onyo kwa watumishi wa idara ya mifugo wa halmashauri hiyo kutokana na kutowajibika kikamilifu na kufanya kulalamikiwa na wafugaji na kumwagiza mkuu wa idara kuwasimamia
watumishi walio chini yake.
Wakizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani la halmashauri hiyo kilichofanyika siku ya ijumaa kwenye ukumbi wa Rutesco, madiwani hao walisema kuwa maafisa ugani wengi wa mifugo walio vijijini hawawajibiki kikamilifu katika kuwahudumia wenye mifugo hali inayosababisha mifugo wengi kufa kwa kukosa huduma ya matibabu pindi wanapougua.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Mohamedi Mtambo alisema kuwa kwenye
halmashauri hiyo hivi sasa idadi ya mifugo hasa ngombe na mbuzi imeongezeka kutokana na miradi mbalimbali kama ya tasaf lakini utoaji wa huduma za matibabu si ya kuridhisha kutokana na maafisa
ugani kushindwa kuwahudumia kwa haraka mara wanapopata taarifa kutoka kwa wenye mifugo, hivyo kufanya idara hiyo ilalamikiwe.
Diwani wa kata ya Mandawa, Rashidi Lipei alisema kuwa hali hiyo isipodhibitiwa mapema uenda ikasababisha milipuko ya magonjwa ya mifugo hivyo alimtaka Afisa huyo kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa utendaji wa kazi wa watumishi walio chini yake na kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wasiotimiza wajibu wao.
“Tatizo la huyo mkuu wa idara amekuwa mlokole sana hivyo upole wake umezidi mipaka.. kwa hali hiyo namtaka aache ulokole na badala yake aweke utaratibu wa kuwakagua maafisa wa ugani wa ngazi mbalimbali kwani wanakuwa kikwazo kwa ufugaji kwenye halmashauri yetu”alisema Lipei.
Alitaja baadhi ya mambo ambayo maafisa ugani hao
wanalalamikiwa ni pamoja na kuchelewa kutoa huduma za matibabu ambapo inawachukua hata baada ya siku tatu kwenda kutoa huduma kwa mfugaji wakati halmashauri imeshawawezesha usafiri wa
pikipiki ambao ulitarajiwa kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakulima.
Kauli ya malalamiko hayo iliungwa mkono pia na diwani wa
kata ya Chinongwe, Fabiani Nguli ambaye alibainisha kuwa kutokana na uzembe wa maafisa hao wa mifugo ilisababisha ng’ombe wa wakazi wa eneo hilo wakiwemo ng’ombe wake watatu kufa baada ya kuchelewa kupatiwa matibabu licha ya kutoa taarifa mapema
kwa afisa ugani wa kata hiyo.
Akizungumzia malalamiko hayo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Reuben Mfune aliwaomba madiwani hao kusimamia kwa ukaribu utendaji wa kazi wa watumishi mbalimbali waliopo kwenya kata zao wakiwemo waafisa ugani wa kilimo na mifugo na kuwa wao ndio wanajukumu kubwa la kuhakikisha watumishi hao watimiza
majukumu yao.