Profesa John Nkoma
VITUO vitano vya televisheni vya hapa nchini vitaonekana kwenye ving’amuzi vya kampuni tatu ambazo zimepewa leseni na Serikali ya kurusha matangazo ya digitali.Dar es Salaam ndio Mkoa wa kwanza kuingia kwenye mfumo huo ambapo jana mitambo ya analojia ilizimwa na itafuatiwa na mikoa ya Dodoma na Tanga Januari 31, Mwanza Februari 28, Moshi na Arusha Machi 31 na Mbeya Aprili 30 mwaka huu.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma alisema makubaliano ya awali ni kampuni hizo tatu kuhakikisha vituo vya televisheni vyenye leseni ya kitaifa vitarushwa.
Vituo hivyo vyenye leseni ya kitaifa ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10 na Star TV ambavyo vitaonekana kwenye ving’amuzi vya kampuni za Star Media (T) Limited, Agape Associates Limited na Basic Transmissions Limited.
“Vituo vingine ambavyo haviko katika makubaliano hayo, matangazo yao yataonekana kwenye ving’amuzi hivyo pale watakapopeleka mawimbi yao kwenye kampuni hizo. “Kwa kuwa leo (jana) ndio siku ya kuzima mitambo ya analojia, hakuna njia nyingine ya vituo hivi zaidi ya kupeleka matangazo yake kwenye kampuni hizo,” alisema.
Vituo hivyo ni pamoja na DTV, Capital TV, Tumaini TV, ATN, Mlimani TV, C2C, CTN, Clouds TV na Efatha. Nkoma aliongeza kuwa baadhi ya kampuni ambazo zinarusha matangazo yao kwa satelaiti au waya kama MultiChoice, Zuku na Easy TV, uonekanaji wa vituo vya televisheni vya ndani utategemea makubaliano kati yao.
Mkurugenzi huyo alitolea mfano kampuni ya MultiChoice ambayo inaonesha matangazo ya kituo cha ndani cha TBC1 pekee baada ya kukubaliana.
Akizungumzia uzimaji wa mitambo ya analojia ya Kisarawe na Makongo, Nkoma alisema hatua kali zitachukuliwa kwa vituo vya televisheni ambavyo havitazima mitambo yao kama walivyoelekezwa.
“Tumeshazungumza na wahandisi wa vituo hivyo kuhakikisha wanabadili matangazo yao, sasa kama kituo chochote hakitatekeleza hilo, sheria zipo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Katika uzimaji wa mitambo hiyo ambayo itagusa maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, Kibaha, Bagamoyo, Kisarawe na Mkuranga, vituo 13 vya televisheni vitabadili matangazo yao kutoka kwenye analojia na kwenda dijitali.
Vituo hivyo ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, Star TV, DTV, Capital TV, Tumaini TV, ATN, Mlimani TV, C2C, CTN, Clouds TV na Efatha.
Akijibu swali la upunguzaji zaidi wa gharama za ving’amuzi, Nkoma alisema mpaka sasa bei ya ving’amuzi imepungua baada ya Serikali kupunguza kodi ya uingizaji wa vifaa hivyo na kuwa suala la kupunguza zaidi liko mikononi mwa Hazina na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Chanzo: Habari Leo