Na. Mwandishi Wetu, Lindi.
Chama cha Soka Mkoa wa Lindi (LIREFA) kilifanya makabidhiano ya msaada kwa klabu bingwa ya mkoa wa Lindi, Mnazi Mmoja Rangers, kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, Machi 5, 2025.
LIREFA ilikabidhi katoni zaidi ya 40 za maji, fedha Tsh 300,000, na mipira mitatu kwa timu hiyo.
Makabidhiano hayo yalifanyika kwa uongozi wa juu wa LIREFA, ukiongozwa na Mwenyekiti CPA Hosseah Hopaje, Mjumbe wa Mkutano Mkuu Rehure Nyaulawa, na Katibu Mkuu Ibrahim Hamisi, walipokwenda kuitembelea timu hiyo mazoezini katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja.
Akizungumza na wachezaji, Mwenyekiti wa LIREFA, CPA Hosseah Hopaje Lugano, alisisitiza umuhimu wa kujituma na kupambana kwa nguvu ili timu hiyo iweze kufikia malengo ya kushika nafasi mbili za juu na kufuzu kwa nane bora, hatua inayoweza kuziwezesha kupanda daraja la pili.
Aidha, LIREFA iliahidi kutoa zawadi kwa kila goli litakalofungwa na timu ya Mnazi Mmoja Rangers katika mashindano haya. Mwenyekiti wa LIREFA, CPA Hosseah Hopaje Lugano, aliahidi kutoa Sh. 200,000 kwa kila goli, huku Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Rehure Nyaulawa, akiahidi Sh. 100,000 kwa kila goli linalofungwa na timu hiyo.