
Na. Mwandishi Wetu, Lindi
Ikiwa zimebaki siku tatu kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Machi 8, 2025, Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi imetoa msaada wa mahitaji muhimu kwa wakazi wa Kata ya Rasbura.
Akikabidhi msaada huo leo, Machi 4, 2025, katika Ofisi ya Kata ya Rasbura, Diwani wa kata hiyo, Mhe. Abdallah Kikwei, aliishukuru kamati kwa msaada wa vitu vinavyosaidia kaya nyingi katika kata yake. Msaada huo unajumuisha mchele, unga, sabuni, sukari, pamoja na mafuta ya kula na kupakaa.
Mhe. Kikwei aliiomba kamati hiyo kuendelea na moyo wa kutoa msaada kwa maeneo mengine yenye uhitaji.
Naye Mtendaji wa Kata ya Rasbura, Abdulmajid Said Murad, aliipongeza kamati hiyo kwa msaada wao, akisema kuwa msaada huo utasaidia kaya nyingi zilizo na uhitaji.
Katika hatua nyingine, mdau wa maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mwatumu Juma Msangi (Mama Kidia), alitoa ufadhili wa bima za Afya Jamii zilizoboreshwa (iCHF) kwa wakazi wa Manispaa ya Lindi kwa kaya 20, zenye jumla ya watu 120. Bima hizo, zenye thamani ya shilingi laki sita, zitasaidia katika matibabu ya wanufaika hao.
Wakipokea bima hizo, wanufaika walimshukuru mdau huyo wa maendeleo kwa kuwapatia bima zitakazowasaidia pindi watakapohitaji huduma za matibabu.