KWA YANGA HII SIMBA IFUNGE NGUO ZIKAZE JUMAMOSI

Jumamosi, Machi 8, rekodi nyingine inakwenda kuandikwa katika mechi za watani wa jadi kati ya Yanga na Simba, zitakapoumana katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 1:15 usiku.

Takwimu za jumla zinaiweka Yanga juu inapokuja kwenye mechi za Dabi ya Kariakoo. Haji Manara, ambaye amewahi kuwa msemaji wa Yanga, anasema kwa kauli maarufu kuwa hakuna timu yoyote iliyofungwa mara nyingi na Yanga duniani kuliko Simba. Hii inadhihirishwa na mechi nne zilizopita ambapo Simba hawajapata ushindi dhidi ya Yanga.

Bahati mbaya kwa Simba, Jumamosi wanakutana na Yanga ambayo inaonekana bora zaidi kuliko nyakati zote, isipokuwa ile ya msimu uliopita walipoibuka na ushindi mkubwa wa mabao 5-1.

Baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu, Yanga ilijipanga upya kwa kumfuta kazi aliyekuwa kocha wake mkuu, Miguel Gamondi, na kumleta Sead Ramovic, maarufu kama 'Germany Machine'. Ramovic alifanya kazi kubwa ya kurejesha utimamu wa wachezaji na licha ya kuanza vibaya michuano ya Ligi ya Mabingwa, Almanusra Yanga ilipindua meza na kufika robo fainali ya michuano hiyo. Ingawa walikosa bahati katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya MC Alger, walilazimika sare ya bila kufungana nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hata alipoondoka Ramovic, kocha mpya Miloud Hamdi ameendeleza falsafa ile ile ya ushindi, na timu yake inaendelea kufunga mabao kama mvua. Mwanzoni mwa msimu, Yanga haikuwa inafunga mabao mengi, lakini sasa ni timu inayoongoza kwa mabao katika ligi, ikiwa imefunga mabao 58.

Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa Yanga ndio timu yenye safu bora ya ushambuliaji, huku utatu wa wachezaji Clement Mzize, Prince Dube, na Stephane Aziz Ki wakiwa wamehusika katika mabao 44 kati ya 58 yaliyofungwa.

Ni wazi kuwa itakuwa mechi ngumu, hasa ikizingatiwa mazingira ya mchezo huo, ambapo matokeo yanaweza kuamua hatma ya ubingwa msimu huu. Lakini Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa ni timu bora zaidi, na litabaki jukumu la wachezaji kudhihirisha ubora wao kwa kushinda.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post