NA MWANDISHI WETU: Ahmeid A.Aziz
MWALIMU mkuu wa Shule ya msingi Rutamba,iliyopo Halmashauri ya Lindi vijijini, mkoani hapa,Yohana Mtila,amejikuta akilazwa nje ya nyumba yake,kwa kile kinachoelezwa ni kutokana na vitendo vinavyodaiwa ni vya kishirikina.
Habari kutoka katani hapo na kuthibitishwa na baadhi ya wananchi,viongozi akiwemo Afisa elimu wake,Cosmas Magigi,zinaeleza kitendo kimefanyika usiku wa Decemba 10 mwaka huu.
Baadhi ya wananchi,wakiwemo na walimu wenzake wamewaambia waandishi wa Habari hizi waliokuwa wametembelea katani hapo kwa lengo la kufuatilia kwa taarifa hizo kwamba,mwalimu Mtira,alikutwa na Juma Abdallah Mbilemoto, akiwa amelala nje eneo la kibao cha Shule hiyo.
Wakielezea zaidi mwalimu wa taaluma,Francise Milanzi,Nambaga Rashidi, na Mohamedi Rwambo,kwa nyakati tafauti walisema asubuhi ya Decemba 11 mwaka huu,Juma Mbilemoto akiwa anamsindikiza Stendi ya magari kijana wake wa kike aliyekuwa akisafiri kwenda Jijini Dar es salaam,walimkuta mwalimu huyo akiwa amelala chini ya kibao cha Shule yao huku akiwa uchi.
“Huyu Juma Mbilemoto alikuwa akimsindikiza kijana wake na walipofika eneo la Kibao cha Shule walimkuta mwalimu mwenzetu akiwa anauchapa usingizi huku akiwa na chupi tu bila ya hata kuwa na Shuka”
“Awali alifikiri ni mlevi amelala,lakini walipomsogelea wakagundua kuwa ni mwalimu na kuanza kumuamsha kwa kipindi kirefu bila ya kuamka,,,,,,lakini walijitahidi na kufanikiwa kuamka na kuanza kushangaashangaa”Alisema mwalimu Nambaga Rashidi.
Rashidi na Rwambo wakinukuu maelezo ya Juma Mbilemoto,alisema baada ya mwalimu huyo kufanikiwa kuamka alimuamuru kijana wake huyo ampatie upande wa kitenge ili aweze kujisitili kuelekea nyumbani kwake, ambapo sio mbali alipokuwa amelazwa mwalimu huyo.
Mwalimu mkuu huyo,Yohana Mtila na Juma Mbilemoto hawakuwa kupatikana ili kupata kauli zao,kwani Mtila alikuwa ameondoka eneo lake la kazi akiwemo na Mbilemoto aliyekuwa amesafiri pia.
Wakizungumza walimu wa Shule hiyo,wamesema wanasikitishwa na kitendo alichofanyiwa mwenziwao cha kulazwa nje ya nyumba yake,na kueleza kimewatia hofu kubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kuhudumu kwenye Shule hiyo.
“Kati ya waliokosa usingizi kwa siku ya jana ni mimi hapa,kwani sikupata usingizi hata kidogo nikifikiria kitendo alichofanyiwa mwenzetu huyu”Alisema Milanzi.
Mwenyekiti wa kamati ya Shule hiyo,Hamisi Omari Mtengeneka,amesema kitendo cha kulazwa nje kwa mwalimu huyo kumechafua sifa ya kata hiyo,ikizingatiwa haijawahi kutokea kitu cha aina hiyo tokea enzi za upigania uhuru wa nchi ya Msumbiji.
Diwani wa kata hiyo, Mendrard Ng’ombo,kwa upande wake alisema hii ni mara ya kwanza kutokea kitendo hicho,tangu kuanzishwa kwake, ikizingatiwa kata hiyo ilikuwa ni moja ya kambi ya wapigania uhuru wa nchi za Msumbiji.
Kata ya Rutamba iliyozalisha vijiji viwili vya Rutamba ya zamani na sasa,ilikuwa ni kambi kwa wapigania uhuru wa nchi za Afrika kusini, ikiwemo ya Msumbiji.
Afisa elimu wa Shule za msingi katika Halmashauri ya Lindi vijijini,Cosmas Magigi alipoulizwa na timu ya waandishi aliyokutananayo Shuleni hapo, kwa upande wake alisema amesikitishwa na kitendo hicho na kueleza kwamba hivi sasa Ofisi yake inafanya utaratibu wa kumuhamishia Shule nyingine.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa kata hiyo,wamedai kitendo cha mwalimu huyo kulala nje ya nyumba yake,kumechangiwa na kitendo chake cha kumchukuwa motto wa mwalimu mwenzake aliyetajwa kwa jina la Machea na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji na kumchanja chale mwilinikwa lengo la kutaka kumsaidia kutoa ushahidi kesi aliyoifungua mahakamni zidi ya Rashidi Michael.
Wakazi hao Issa Penda na Juma Choteka, walisema mwalim Mtila amefungua kesi zidi ya Raishidi Michael,akidai alipwe fidia kutokana na kitendo cha kumjeruhi mbuzi wake kwa panga ubavuni kufuatia mbuzi huyo kula unga wake.
“Huyu mwalimu Mtila amefungua kesi mahakamani akitaka alipwe fidia kwa kuuwawa kwa mbuzi wake kwa kuchomwa panga ubavuni na Rashidi Michael,akidai ya kula unga wake,,,,,,,watoto wawili akiwemo na huyo aliyemchukuwa kwenda naye kwa mganga walishuhudia wakati Michael, akimrushia mbuzi huyo panga na kumchoma mbavuni,,,,,,,,hivyo alimchukuwa motto wa mwalimu huyo na kwenda naye kwa mganga na kuchanjwa chale bila ya mzazi wake kufahamishwa”Walisema wakazi hao.
Walisema kitendo cha mbuzi wake kuchomwa panga alilazimika kwenda Ofisi ya Serikali ya Kijiji na hatimaye kituo cha Polisi kata ya Rutamba, ambapo aliombwa kuyamaliza,lakini mwalimu huyo hakuweza kukubali na kufungua kesi ya madai mahakamani dhidi ya mbuzi wake.
“Mtoto huyo ana asili ya ulilo,sasa kitendo cha kumchukuwa kwenda kwa mganga kumchanja chale mwilini ili amsaidie kutoa ushaihidi mahakamani bila ya kumtaarifu mzazi wake,na aliporejea nyumbani alionekana mwili mzima umevimba, na alipoulizwa yule kijana akaeleza na ndipo mwalimu yule akapewa adhabu mbili ya kulipa Sh,80,000/- na kwenda kugalauka kwenye kilinge”Walisema wakazi hao.
Aidha, wakazi hao walisema iwapo mwalimu huyo asipotekeleza masharti hayo,bado mzimu huo utaendelea kumuandama hata kama angekwenda nje ya mkoa wa Lindi na nchi kwa ujumla.
Waandishi hawakufanikiwa kuwapata Rashidi Michael na mwalimu Machela,ili nao kupata kauli zao baada ya kuelezwa wote kwa pamoja wamesafiri nje ya kata hiyo,hata hivyo jitihada za kuwapata wahusika hao zinaendelea ili kupata kauli zao.
Hili ni tukio la pili kutokea katika Halmashauri ya Lindi vijijini, kwani mwezi Februari mwaka huu, mwalimu wa Sekondari ya molela,aitwae Chacha naye alikutwa amelazwa nje kwenye Kibao cha Shule hiyo akiwa uchi wa mnyama.