NA Mwandishi Wetu: Ahmeid A.Azizi
WATU wasiojulikana wameiba pikipiki moja iliyokuwa imeazimwa na askari Polisi wa kituo cha kata ya Rutamba,wilaya ya mkoa wa Lindi,aliyefahamika kwa jina la Juma,wakati yeye na wenzake wakiwa katika Doria, eneo la kata na Tarafa ya Rondo,wilayani humo.
Pikipiki hiyo aina ya Tibeter ni mali ya mfanyakazi wa Idara ya Afya kituo cha Rutamba aitwae Jenny Ruoga,iliazimwa na askari huyo kutoka kwa mwendesha bodaboda aitwae Juma Chapindo.
Habari kutoka kata hiyo na kuthibitishwa na dereva wa Bodaboda hiyo,Juma Chapindo na mmiliki wa pikipiki hiyo aina ya Tibeter,Jenny Ruoga na Juma Chapindo,zinaeleza pikipiki hiyo,imeibiwa usiku wa Decemba 10 mwaka huu,kijiji cha Ntene,kata ya Rondo.
Baadhi ya wakazi wa Rutamba ambao hakutaka majina yao yatajwe wakihofia kufuatwa fuatwa na askari hao,walisema siku hiyo askari Polisi Juma akiwa na wenzake wawili,akiwemo waliyemtaja kuwa ni Bahati, walimuuomba amuazime pikipiki yake kwa ajili ya kwenda kata ya Rondo kufanyia Doria.
Walisema mwendesha Bodaboda huyo alimkatalia,lakini kutokana na nguvu za ki-askari aliendelea kumshawishi ili ampatie na hatimaye kukubali kumkabidhi na yeye kubaki nyumbani akiendelea kupumzika.
Kwa upande wake mwendesha bodaboda Juma Chapindo, ameliambia gazeti hili kwamba,ilipofika siku ya pili yake,yaani Decemba 12/2012,akiwa nyumbani akisubiri kifaa chake hicho cha kazi,alijiwa na mmoja wa madereva mwenzake na kumueleza anatakiwa kituo cha Polisi kata ya Rutamba.
“Nilipoambia naitwa kituoni nilistuka kidogo na kujiuliza naitiwa kitu gani,kwani pikipiki yangu nilishailipia kila kitu, leo naitiwa kitu gain Polisi”Alisema Chapindo.
Chapindo alisema aliamua kwenda kituoni hapo na kumkuta askari aliyekuwa amemuazima pikipiki yake pamoja na wenzake na kumuelezea tukio walilolipata,hali ambayo ilimpa wakati mgumu,ikizingatiwa chombo hicho sio mali ya kwake.
“Siku hiyo ya tarehe 11 usiku alinijia askari Juma na kuniomba nimuazime piki akafanyie doria kijiji cha Ruponda,Rondo,nikamkatalia,,,,,,,,lakini akaendelea kuning’ang’ania nikalazimika kumpa”
“Ilipofika siku ya pili yake,nikiwa nyumbani akaja mwendesha bodaboda mwenzangu (hakumtaja jina) ambaye naye alikuwa katika kundi la kuazimwa pikipiki zetu na kuniambia naitwa kituo cha Polisi,,,,,,,nilishutuka mno na kujiuliza kulikoni”Alisema Chipindo.
Alisema alipofika katika kituo hicho,alikutana na askari Juma akiwa na wenzake na kumueleza kuibiwa kwa pikipiki yake,tukio ambalo lilimpa wakati mgumu asiujue la kufanya akizingatia kuwa sio mali yake,huku akipewa imani ya kupatikana kwake.
Chipindo akasema akiwa nyumbani kwake akiendelea kutafakari nini afanye,alifikiwa na tajiri yake huyo,Jeny Ruoga na kulazimika kumueleza hali halisi ya tukio la kuibiwa kwa pikipiki yake kutoka kwa askari Polisi Juma.
Kwa upande wake mmiliki wa pikipiki hiyo,Jenny Ruoga amethibitisha kuibiwa kwa pikipiki yake hiyo ambayo hakuweza kutaja namba zake za usajili,kufuatia kupewa taarifa ya kuibwa kwa chombo chake na mchumba wake aitwae Said Sharifu.
“Taarifa ya kuibiwa kwa pikipiki yangu nilipata kutoka kwa mchumba wangu Said Sharifu,,,,,,,,,,,,Sikuweza kuamini nikaamua kwenda nyumbani kwa Dereva wangu,ambaye kwa siku hiyo alikuwa akisumbuliwa na homa” Alisema Ruoga.
Ruoga ambaye ni mtumishi wa Idara ya Afya kituo cha Rutamba,ameitaja namba ya Chensesi ya pikipiki yake hiyo aina ya Tibeter kuwa ni, ZENCJLFXA 6816386.
Waandishi wa habari walipotaka kufahamu hatima yake iwapo haitaweza kupatikana, alijibu kwa kusema gharama ya kuilipa ni ya dereva wake Juma Chipando,kwani ndiye aliyemkabidhi kufanyia kazi kwa ajili ya kujiongezea kipato yeye na dereva wake huyo.
“Nimeambiwa kuna asilimia 90% uwezekano wa kuipata kwa pikipiki yangu ndani ya wiki moja,lakini kama haikupatikana basi dereva itabidi anilipe fedha zangu zote tena taslimu na sio nusunusu ili niweze kununua nyingine”Alisema Ruoga.
Asakari Polisi Juma wa kituo hicho cha Rutamba,hakuweza kupatikana ili kusikia kauli yake, baada ya kuelezwa amesafiri nje ya kata hiyo ya Rutamba,huku baadhi ya askari wenzake wakikataa kuzungumzia tukio hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi,George Mwakajinga alipoulizwa juu ya tukio hilo,amesema Ofisi yake haina taarifa hiyo, na kuhaidi kufuatilia ili kuweza kupata ukweli wake.