NIJUZE NIJUZE Author
Title: KATIBU WA ZAMANI WA SIMBA HASANOO KORTIN KWA WIZI WA PEMBE ZA NDOVU
Author: NIJUZE
Rating 5 of 5 Des:
MWENYEKITI wa Chama cha Soka Pwani (Corefa), Hassani Othman maarufu kama Hasanoo (43) na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakamaya...
MWENYEKITI wa Chama cha Soka Pwani (Corefa), Hassani Othman maarufu kama Hasanoo (43) na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakamaya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la uhujumu uchumi na kusafirisha pembe za ndovu (Meno ya Tembo)   kutoka Dar es Salaam kwenda Hong Kong, yenye thamani ya Sh1.1 bilioni.
Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro jana aliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando kuwa ni Ally Kimwaga, Dastan Mwanga, Godfrey Mwanga, John Mlai na Khalid Fazaldin.
Kimaro alidai katika shtaka la kwanza kuwa, kati ya Septemba Mosi na Novemba 20, mwaka huu, Dar es Salaam na Hong Kong kinyume na kifungu cha 384 ya kanuni ya adhabu sura ya 16.
Amesema washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kujihusisha na biashara ya nyara za serikali bila ya kuwa na leseni inayowaruhusu kufanya hivyo.
Katika shtaka la pili, Kimaro alidai kuwa kati ya Septemba Mosi na Novemba 20, mwaka huu, Dar es Salaam na Hong Kong washtakiwa hao kwa nia ovu walipanga, wakatekeleza, wakasimamia na kuwezesha kifedha kufanyika kwa biashara ya nyara za serikali kwa kusafirisha vipande 569 vya Pembe za ndovu, vyenye uzito wa kilogramu 1330 na thamani ya Sh 1,185,030,000 kwenda Hong Kong.
Wakili huyo wa Serikali, katika shtaka la tatu alidai kuwasiku hiyo ya tukio washtakiwa hao walijihusisha na biashara ya nyara za serikali kinyume na kifungu cha 80 na 34 ya uhifadhi wa Wanyama Pori namba 5.

Aliongeza kwa kudai kuwa, washtakiwa hao kwa nia ovu waliendesha biashara hiyo ya nyara za serikali bila ya kuwa na kibali halali kinachowaruhusu kufanya biashara hiyo.
Baada ya kuwasomea washtakiwa hao mashtaka, Hakimu Mmband aliwaambia washtakiwa hao kuwa, kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi, Ritha Tarimo ambaye hayupo na kwa sababu hiyo, hawaruhusiwi kuongea chochote kwa sababu hati ya mashtaka haijaambatanishwa na hati kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Wakili Kimaro alidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mmbando aliiahirisha kesi hiyo, hadiJumatano ya Novemba 28, mwaka huu itakapotajwa.
Mbali na kesi hiyo, Hasanoo aliyewahi kuwa kiongozi wa Simba pia anakabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa tani 26.475 za madini aina ya Shaba zenye thamani ya Sh333, 467,848.13 kutoka Zambia kinyume na kifungu cha 258, 265 na 269 (c) vya kanuni ya adhabu mali ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania Ltd

About Author

Advertisement

 
Top