Unknown Unknown Author
Title: YANGA YAPIGWA 1-0 KAITABA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
BAO pekee la Themi Felix katika dakika ya 67, jioni ya leo limewapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba...
BAO pekee la Themi Felix katika dakika ya 67, jioni ya leo limewapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
Hiyo inakuwa mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba SC.

Aidha, hii ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.  
Kwa ujumla Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa, ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na leo imechapwa 1-0 na Kagera Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.
Katika mechi hiyo, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati ya hayo kwa penalti. 
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Omar Juma kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Dominick Nyamsana wa Dodoma na Hassan Zani wa Arusha, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma Abdul, Stefano Mwasyika/nurdin, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi/Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
Kagera; Andrew Ntala, Jumanne Nade, Salum Kanoni, Amandus Nesta, Benjamin Effe, Malegsesi Mwangwa, Daudi Jumanne, George Kavilla, Enyinna Darlington/Themi Felix, Shijja Mkinna na Wilfred Emmeh/Paul Ngway.







About Author

Advertisement

 
Top