NIJUZE NIJUZE Author
Title: TAARIFA KUTOKA TFF LEO
Author: NIJUZE
Rating 5 of 5 Des:
SIMBA, WAGANDA SASA KUCHEZA JUMAPILI Mechi ya Simba na URA ya Uganda kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) iliy...
SIMBA, WAGANDA SASA KUCHEZA JUMAPILI
Mechi ya Simba na URA ya Uganda kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) iliyokuwa ichezwe Jumatatu (Julai 16 mwaka huu) sasa itafanyika Jumapili (Julai 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limefanya mabadiliko hayo kutokana na fainali ya Copa Coca-Cola 2012 iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo kuhamishiwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Kutokana na mabadiliko hayo, mbali ya mechi ya Simba na URA itakayoanza saa 10 kamili jioni, mechi nyingine Jumapili itakuwa kati ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) dhidi ya Ports ya Djibouti itachezwa saa 8 kamili mchana Uwanja wa Chamazi.
Pia siku hiyo hiyo ya Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi nyingine itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi hiyo itazikutanisha timu za Azam ya Tanzania Bara na Mafunzo kutoka Zanzibar.
Mechi za ufunguzi wa mashindano hayo Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitabaki kama zilivyopangwa awali. Mechi ya kwanza saa 8 mchana itakuwa kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya Sudan Kusini wakati saa 10 kamili jioni Yanga itaoneshana kazi na Atletico ya Burundi.VIINGILIO MICHUANO YA KAGAME 5,000/- KWA 2,000/-

Viingilio vya chini katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayoanza Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) vitakuwa sh. 5,000 kwa mechi za Yanga na Simba, na sh. 2,000 kwa mechi ambazo hazihusishi timu hizo. Yanga ni bingwa mtetezi wakati Simba ni makamu bingwa mtetezi.
Kwa upande wa mechi zinazohusisha Yanga na Simba viingilio vitakuwa kama ifuatavyo; viti vya bluu na kijani sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, viti vya VIP C sh. 10,000, viti vya VIP B sh. 15,000 na viti vya VIP A ni sh. 20,000.
Siku ambazo Simba na Yanga hazichezi, viingilio vitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya VIP C, sh. 10,000 kwa viti vya VIP B na sh. 15,000 kwa viti vya VIP A. Mshabiki akikata tiketi moja anaona mechi zote mbili; mechi ya saa 8 na ile ya saa 10.
Timu za El Salam Wau ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi zimewasili Dar es Salaam jana usiku (Julai 11 mwaka huu) tayari kwa mashindano hayo wakati nyingine zote zilizobaki kutoka nje zinawasili leo katika muda tofauti.
TEMEKE, MWANZA ZAVAANA NUSU FAINALI COPA 2012
Temeke na Mwanza zinapambana kesho (Julai 13 mwaka huu) katika nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 itakayochezwa saa 2.30 asubuhi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nusu fainali ya pili itaanza saa 9.30 mchana kwenye uwanja huo huo ikizikutanisha timu za Morogoro na Tanga.
Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na fainali ya michuano hiyo zitachezwa Jumapili (Julai 15 mwaka huu). Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 5 asubuhi na kufuatiwa na fainali ambayo itafanyika kuanzia saa 9 kamili alasiri.
Mwanza ilipata tiketi ya nusu fainali kwa kuifunga Kinondoni 3-1 huku Temeke ikitinga hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Mjini Magharibi. Ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mara ndiyo ulioipa Morogoro tiketi ya nusu fainali wakati Tanga yenyewe iliilaza Dodoma bao 1-0.
TWIGA STARS YASAIDIWA VIFAA VYA MIL 1.3/-
Kampuni ya bima ya Maxinsure imetoa vifaa vya mazoezi kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) vyenye thamani ya sh. milioni 1.3.
Vifaa hivyo ambavyo ni jezi, bukta na soksi 20, vizibao (bibs) 20 na mipira miwili vimekabidhiwa leo (Julai 12 mwaka huu) kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Amisa Juma.
Akikabidhi vifaa hivyo, Amisa amesema wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa jamii lakini vilevile wameamua kuiunga mkono timu hiyo ambayo wanajua haina mdhamini kutokana na vipaji na uwezo ambao umekuwa ukioneshwa na wachezaji wake.
Pia amezitaka kampuni, taasisi, watu binafsi na Serikali kuiunga mkono timu hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali inayotarajia kushiriki.

Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top