KOCHA wa Yanga, Kosta Papic amerudia wito wake na kuwaangukia mashabiki wa Simba kutoishangilia Zamalek katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga itacheza na Zamalek inayowasili leo katika mchezo wao kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku mashabiki wa Simba wakiahidi kuwashangilia Wamisri hao tangu filimbi ya kwanza ya mchezo huo.
"Sijawahi kuona sehemu yoyote mashabiki wakishangilia timu ya nje, kwa mara ya kwanza naiona hapa Tanzania," alisema Papic ikiwa ni siku moja baada ya mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage kusema 'ruksa' Simba kuishangilia Zamalek kwani hawezi kuzuia mapenzi ya mtu.
"Ninawaomba mashabiki wa Simba wasifanye hivyo, ninawaomba sana. Ni vizuri waje uwanjani wakae kimya na si kushangilia wapinzani wetu," alisema Mserbia huyo.
Jana mitaa ya kariakoo mashabiki wa Simba walionekana kwa wingi wakinunua kwa kasi jezi za klabu hiyo ya Misri wakidai ni malipizo baada ya Yanga kununua kwa fujo jezi za TP Mazembe walipocheza na Simba mwaka jana katika michuano hiyo.
"Hata mashabiki wa Manchester United huwa hawaishangilii AC Milan inapocheza na Arsenal kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, badala yake huwa wanakaa kimya tu na kwenda kushangilia nyumbani," alisema Papic.
Alisema katika nchi zote za Afrika alizofundisha soka kama Nigeria, Ghana na Afrika Kusini hajawahi kuona wenyeji wakiishangilia timu ngeni. "Hata Zamalek wenyewe watashangaa kuona wakishangiliwa, wataona hatuna umoja. Tunaposema mshikamano na umoja, lazima tuanze kwenye michezo na si vinginevyo," alisema.
Katika hatua nyingine, Papic alisema atatumia mtindo wake wa kushambulia kama kawaida katika mchezo huo.
"Hatujacheza vizuri sana katika mechi za Ligi Kuu Bara, lakini hilo haliwezi kunifanya kubadilisha mfumo wangu, nitacheza kwa kushambulia kama kawaida.
"Ni mechi ngumu na hatuwezi kukatishwa tamaa kwa vyovyote, tunakwenda kupigana," alisema.
Pamoja na hayo, alisema timu yake inakabiliwa na majeruhi wengi kiasi ambacho kinamfanya asijue timu itakavyo kuwa. "Timu ina majeruhi wengi ambao ni Geoffrey Bonny, Rashid Gumbo, Yew Berko na Salum Telela, wachezaji wa kikosi cha kwanza wakiwa majeruhi ni dalili mbaya katika timu," alifafanua Kocha huyo Raia wa Serbia.
Uongozi wa Yanga umesema una matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo wake wa kesho wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.
Papic hana matumaini na kikosi chake kama kitaweze kukabiliana na wapinzani wao kutokana kutoridhika na kiwango cha maandalizi ya timu hiyo hadi hivi sasa.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Emmanuel Nchimbi amewatakia kila la heri Yanga katika mechi yao ya kesho dhidi ya Zamalek ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Nawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi kuipa Yanga sapoti kwani mashabiki ni mchezaji wa 12, hii itawahamasisha wachezaji kuwa na morali na hatimaye kushinda mechi hiyo," alisema Nchimbi.