NIJUZE NIJUZE Author
Title: JK apinga hoja zote Chadema
Author: NIJUZE
Rating 5 of 5 Des:
RAIS Jakaya Kikwete emesema licha ya kelele za wanasiasa, atasaini Sheria ya mchakato wa kuunda Katiba Mpya. Alitoa kauli jana na kupangua h...

imageRAIS Jakaya Kikwete emesema licha ya kelele za wanasiasa, atasaini Sheria ya mchakato wa kuunda Katiba Mpya.
Alitoa kauli jana na kupangua hoja zote kupinga mchakato huo zilizotolewa na Chadema kwamba muswada huo haukuzingatia kanuni zitakazowezesha demokrasia.Kauli hiyo ya Rais imekuja saa chache baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Mabadiliko ya Katiba ambao ulisusiwa na Wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi kwa madai kuwa mchakato mzima una kasoro.
Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa PTA, Sabasaba juu ya hali ya uchumi nchini na mchakato wa Katiba, Rais Kikwete alisema atatia saini sheria ya mchakato wa kuunda katiba mpya ambayo inatokana na muswada uliopitishwa na Bunge jana.
Alikibebesha lawama nyingi Chadema kwa kile alichosema ni upotoshaji wa mchakato huo kwa lengo la kuuvuruga wakati unaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Alimtupia shutuma za waziwazi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema amekuwa kigeugeu kwa sababu mwanzo alimsifu (Rais Kikwete), kwa kukubali Katiba kubadilishwa lakini baadaye akageuka na kuanza kumponda.
“Mbowe ni miongoni mwa watu walionimwagia sifa baada ya kutangaza nia yangu ya kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya, nakumbuka ilikuwa Februari 11, mwaka huu wakati akichangia hotuba yangu katika Kikao cha Bunge alisema: ‘Tunampongeza Rais katika suala hili.’ Ila muda mfupi baadaye chama chake kikaja na mtizamo tofauti wa kunyang’anywa hoja yao… na kwamba Rais asiunde tume wala kuhusika katika mchakato.”
Alisema alishangazwa na kauli za Chadema na kusema: “Hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu kufanya zoezi la marekebisho ya Katiba na hata kuandika Katiba Mpya.”
Alisema kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, katika suala la upatikanaji wa Katiba anayeunda tume ni Rais na akisema hata katika utawala wa Awamu ya Kwanza na ya Pili, ilibadilishwa mara tatu na Rais ndiye aliyeunda tume.
“Mwaka 1977 yalifanyika mabadiliko mengine ya Katiba ambayo yalitengeneza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ilikuja kufanyiwa marekebisho makubwa mwaka 1984,” alisema Rais Kikwete.
Mwaka 1991 na 1992, alisema iliundwa tume nyingine iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali ya kukusanya maoni ya Katiba ya kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi.
“Tume hii ilipendekeza sheria 40 zifutwe, zilifutwa na nyingine zinaendelea kufutwa ikiwemo sheria ya kumweka mtu kizuizini,” alisema.
Alisema mwaka 1997 katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa aliundwa Tume ya Jaji Kisanga ambayo ilikusanya maoni ya mabadiliko ya 13 na 14 ya Katiba.

“Siku zote katika mchakato wa Katiba, tume huundwa na Rais, sasa iweje sasa?... Rais amepungukiwa sifa kikatiba?” alisema na kusisitiza kwamba ndiye mwenye mamlaka kikatiba kuunda kamati hiyo.
Alisema iwapo Chadema kitaandaa mchakato wake wa kuunda katiba itabidi mawazo yao wayakabidhi kwa kamati atakayoiunda.

Alisema tayari CUF iliwasilisha rasimu yake ya Katiba na kuikabidhi serikalini na kwamba nayo itapelekwa kwenye kamati kama sehemu ya maoni yaliyotolewa na makundi ya Watanzania.

Rais alisema uteuzi wa wajumbe katika tume utazingatia sifa na kwa mujibu wa kanuni akisema hana mamlaka ya kuichagua kwa kuzingatia vigezo vya urafiki.

Isitoshe, alisema kitendo chake cha kuridhia mabadiliko ya Katiba nchini kwa sasa hakina maana kwamba iliyopo haifai. Alisema iliyopo imeiongoza vizuri nchi na kuwa kwenye utulivu na amani kwa miaka 50, hivyo haipaswi kuonekana kuwa haifai: “Lengo la kutaka mabadiliko hayo ya Katiba ni kuunda mpya itakayoendana na matakwa ya Watanzania katika wakati huu ambao wanatimiza miaka 50 tangu uhuru wao.”

Alisema Katiba itakayoundwa itajumuisha mawazo ya Watanzania wote ili kuhakikisha kuwa italiongoza vyema taifa katika miaka mingine 50 likiwa tulivu na lenye mshikamano.

Rais kuwa dikteta
Alisema kauli kuwa anaongoza kwa kutumia mtindo wa kidikteta ni za kizushi akisema endapo ingekuwa hivyo, angewatia kizuizini watu wengi ambao wanatoa hoja za kupotosha mambo yanayotendwa na Serikali yake.

Badala yake alisema amekuwa mvumilivu wa yote kwa kuwa anajua wazi katika nchi inayoongozwa kidemokrasia, lazima kuwepo na tofauti za mawazo. Alisema angekuwa hivyo, hata wanaomwita dikteta wasingethubutu kutamka hayo maana wangekamatwa na kutiwa kizuizini au kupotea katika mazingira utata.

Alikigeuzia kibao Chadema akisema kama ni udikteta basi ndicho chenye sifa hiyo kwa kuwa viongozi wake wamekuwa hawataki kuzingatia demokrasia kwa kulazimisha mambo.

Alisema kuwa amekuwa akishangazwa na kauli za Chadema akitoa mfano wa iliyotolewa na chama hicho kuwa kama Katiba mpya haitaandikwa kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao 2015... “Patakuwa hapatoshi.”

Akasema lakini hata pale alipokubali mchakato wa kuunda katiba hiyo kabla ya mwaka 2015, ili ‘patoshe’ bado Chadema kimekuja na kauli nyingine mchakato huo ukiendelea kuwa “Patakuwa hapatoshi.”

Katiba Mpya

Rais Kikwete alisema Katiba mpya itapokea mawazo yote ya wananchi na baada ya kupitishwa kwa rasimu yake na itapelekwa kwa wananchi ili waipigie kura ya kuikubali au kuikataa.
Alisema hiyo ni demokrasia ambayo hata kwenye michakato iliyoendeshwa na Serikali za awamu zilizopita hawakufanya hivyo.
Hali ya Uchumi
Rais Kikwete alisema kuwepo kwa mfumuko wa bei ya vyakula nchini, kushuka kwa thamani ya shilingi na kupanda kwa gharama za maisha kunatokana na kutetereka kwa uchumi wa dunia.

Alisema hali hiyo siyo tu imeiathiri Tanzania, bali hata nchi tajiri kwa sasa hasa barani Ulaya.Alisema Serikali yake inajitahidi kwa kila hali kuhakikisha inatatua yale ambayo yamo ndani ya uwezo wake katika kupunguza makali ya maisha kwa wananchi.

source:mwananchi comunication.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top