Na. Mwandishi Wetu, Ruanggwa
Waziri Mkuu na Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa, amewaaga rasmi wakazi wa jimbo hilo huku akimkabidhi kijiti cha uongozi wa kisiasa mgombea mpya wa CCM, Kasper Mmuya.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za CCM mkoa wa Lindi uliofanyika katika viwanja vya Likangala, Majaliwa aliwataka wananchi kumpa Mmuya ushirikiano wa dhati na kusisitiza kuwa ataendelea kushirikiana naye katika safari ya kuendeleza maendeleo ya Ruangwa.
Katika hotuba yake, alieleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita na kuwakabidhi wagombea wote wa ubunge na udiwani ilani ya CCM, akihimiza kuendeleza dira ya chama hicho.

Kwa upande wake, Kasper Mmuya aliahidi kuendeleza miradi iliyoanzishwa na Majaliwa badala ya kuanzisha mipya, akitaja kipaumbele chake kuwa ni umaliziaji wa barabara ya Nanganga–Ruangwa na utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Wananchi waliopata nafasi ya kujitokeza kwa wingi walimpongeza na kuonesha imani kuwa Mmuya ataendeleza kasi ya maendeleo, tukio ambalo limeacha kumbukumbu muhimu katika historia ya kisiasa ya Ruangwa.

