MAJALIWA AWATAHADHARISHA WAGOMBEA WA CCM KUTOBWETEKA

 Kassim Majaliwa Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) akiongea na Wananchi wa Nachingwea katika uzinduzi wa kampeni za wagombea wa ubunge na udiwani kwa chama cha CCM.

Na Ahmad Mmow, Nachingwea.

Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewatahadharisha wanachama wa chama hicho wasibweteke kusaka kura.

Mheshimiwa Majaliwa ambae pia ni waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa tahadhari hiyo mjini Nachingwea alipozindua kampeni za wagombea wa ubunge na udiwani wanatokana na Chama Cha Mapinduzi.

Amesema wanachama, na wagombea wa chama hicho ambao wamekosa wapinzani kutoka katika vyama vya upinzani kwenye majimbo na kata wanazogombea wasibweteke kusaka kura. Kwani sheria mpya katika uchaguzi zimebadilika.

Waziri mkuu Majaliwa amebainisha kwamba kama ingekuwa sheria ya zamani ni dhahiri wagombea hao wangetangazwa kwamba wameshinda. Hata hivyo sheria mpya inawataka wapigiwe kura.

Kwakuzingatia ukweli huo, Majaliwa ametoa wito kwa wagombea hao na wanachama wa chama hicho wasake kura kwa nguvu zote.

"Tufute na kuomba kura nyumba kwa nyumba,"
Majaliwa alisisitiza.

Katika kusisitiza tahadhari hiyo alisema kwa takwimu zilizopo Tume Huru ya Uchaguzi zinaonesha kwamba wilaya ya Nachingwea inajumla watu 178,000 waliojiandikisha kupiga kura. Ambapo idadi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi katika wilaya hiyo ni takribani  58,000. Kwahiyo kuna wapiga kura 120,000ambao sio wanachama wa chama hicho.

Aidha alitoa wito kwa wagombea ubunge wa majimbo ya Nachingwea na Ruangwa (Fadhily Liwaka jimbo la Nachingwea na Caspar Mmuya wa jimbo la Ruangwa) waendeleze na kusimamia mipango na miradi ambayo ilifanywa na kuanzishwa na watangulizi wao pindi wakichaguliwa kuwa wabunge.

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa maji wa kutoka Nyangao ambao utavinufaisha pia vijiji kumi vilivyopo katika wilaya ya Nachingwea.

Aliutaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Nanganga kwenda Nachingwea.

Mbali ya hayo, mjumbe huyo wa halmashauri kuu ya taifa aliwaasa wagombea wanaotokana na chama hicho wakawaeleze wananchi mazuri na mema yaliyofanywa na chama hicho. Lakini pia wakawaeleze watawafanyia nini pindi wakichaguliwa.

Kwa upande wake mgombea ubunge kupitia chama hicho katika jimbo la Nachingwea, Fadhily Liwaka aliyataja mambo matatu ambayo ataanza kushughulikia iwapo atachaguliwa kuwa mbunge.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni migogoro ya wafugaji na wakulima,  ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Masasi kwenda Nachingwea na mabweni katika shule za sekondari kwa ajili wanafunzi wa kike.

Katika jimbo la Nachingwea mgombea wa ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Fadhily Liwaka hana mshindani.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post