Mama Salma Rashid Kikwete amechukua rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Mchinga, Mkoa wa Lindi, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Tukio hilo limefanyika katika ofisi za Manispaa ya Lindi, mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ya Lindi Mjini na Mchinga, Ndugu Saidi Farhan, likishuhudiwa na wanachama wa CCM waliomsindikiza kwa hamasa kubwa na shangwe.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mama Salma ameahidi kuendeleza jitihada za kuwatumikia wananchi wa Mchinga kwa uadilifu na bidii, huku akiwataka wanachama wa chama hicho kushikamana na kuvunja makundi ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM.
Wanachama kadhaa wa CCM Jimbo la Mchinga walieleza matumaini yao makubwa kwa Mama Salma, wakibainisha kuwa wanasubiri kwa hamu ushindi wake ili aweze kuwatumikia kwa karibu zaidi.
