KATIBU TAWALA MKOA WA LINDI APOKEA TUZO YA PONGEZI

Kamati ya Uratibu ya Maandalizi ya Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Mkoa wa Lindi 2025 imemkabidhi tuzo ya pongezi Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary, kama ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kufanikisha maandalizi ya maonesho hayo.

Tukio la kukabidhi tuzo hiyo limefanyika leo Agosti 26, 2025, ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu, Ndugu Mwinjuma Mkungu, akiambatana na baadhi ya wajumbe wa kamati, alimkabidhi rasmi Bi. Omary heshima hiyo. Tuzo hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza wakati wa kilele cha maonesho yaliyofanyika Juni 2025 wilayani Ruangwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ndugu Mkungu alieleza kuwa tuzo hiyo ni sehemu ya utaratibu wa kamati kutambua na kuthamini mchango wa wadau mbalimbali, ikiwemo mashirika, taasisi na viongozi waliowezesha kufanikisha maonesho hayo. Miongoni mwa waliotunukiwa tuzo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, ambaye ndiye mwasisi wa maonesho hayo makubwa ya mkoa.

“Tunakukabidhi tuzo hii kama ishara ya heshima na shukrani kwa mchango wako na maelekezo yako yaliyowezesha Maonesho ya Madini Mkoa wa Lindi 2025 kufanyika kwa kiwango cha juu na ubora mkubwa,” alisema Mkungu.

Kwa upande wake, Bi. Zuwena Omary alitoa shukrani zake kwa kamati hiyo kwa hatua ya kuthamini mchango wake, akisisitiza kuwa mafanikio ya maonesho hayo yametokana na mshikamano wa pamoja kati ya viongozi, wadau na wananchi wa Mkoa wa Lindi.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post