Afisa Sheria Mwandamizi, Idara
ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.
Ramadhani Myonga, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa wilaya
ya Butiama, mkoani Mara, yaliyotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na
Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS,
NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
CRDB, TCB, NMB na NBC.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo
ya elimu ya fedha wakazi wa Kijiji Kyankoma, Kata ya Nyamimange, Wilaya
ya Butiama, mkoani Mara, wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha yenye
mada mbalimbali ikiwemo masuala ya mikopo, akiba na uwekezaji
yaliyotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi nyingine za Serikali
ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za
Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), CRDB, TCB, NMB na NBC.
Na. Josephine Majura, WF, Mara.
Wakopaji
wametakiwa kutojihusisha na matumizi ya dhamana za mali za familia bila
ridhaa ya familia husika ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea iwapo
mali hizo zitapotezwa kutokana na kushindwa kulipa mikopo.
Afisa
Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, ameyasema hayo wakati wa
mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa kwa wananchi wa Kijiji cha
Kyankoma, Wilaya ya Butiama mkoani Mara na Wizara ya Fedha kwa
kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya
Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki, ikiwemo Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC.
“Wakopaji
wanatakiwa kuwa waangalifu na kuhakikisha wanaelewa masharti ya
mikataba ya mikopo kabla ya kutumia mali ya familia kama dhamana ili
kuhakikisha kuwa dhamana zinazotolewa hazihatarishi ustawi wa familia”
alisema Bw. Myonga.
Aliongeza
kuwa Taasisi za kifedha zinatakiwa kuwa waangalifu na kufuata sheria na
taratibu stahiki kabla ya kukubali mali ya familia kuwekwa kama
dhamana, kwa kuhakikisha kuwa hati zote muhimu, kama vile hati za
umiliki na ridhaa za maandishi za familia husika vinaambatishwa.
Akizungumzia
kuhusu udhamini wa mkopo, Bw. Myonga, waliwashauri wananchi kabla ya
kukubali kuwa wadhamini, wahakikishe wamejiridhisha kuwa mkopaji ana
uwezo wa kulipa mkopo kwa wakati.
Alifafanua
kuwa mtu akiwa mdhamini, anakuwa na wajibu wa kulipa mkopo wote endapo
mkopaji atashindwa kulipa jambo ambalo linaweza kuathiri mali zake
binafsi na hali yake ya kifedha.
Kwa
upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama
mkoani Mara, Bi. Rebeca Sanga, aliwasisitiza wanavikundi wote nchini
kusimamia vizuri miradi waliyonayo ili izalishe faida kwa ajili ya
manufaa ya kundi na mtu mmoja mmoja.
Aliongeza
kuwa miradi ya kikundi ikisimamiwa vizuri itazalisha faida ambayo
inaweza kutumika kama mtaji wa kukopeshana wanakikundi na kujiepusha na
mikopo yenye riba kubwa.
Naye
mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha Bw. Bryan Mkurya,
aliiomba Serikali kuendelea kutoa elimu hiyo katika ngazi zote kuanzia
Kitongoji hadi Kata ili kuhakikisha kila mwananachi anapata elimu ya
fedha.
Aliongeza
kuwa Serikali ihakikishe inatoa elimu kwa mkopaji na mkopeshaji ili
wote wawe na uelewa wa pamoja ili kupunguza migogoro inayoendelea
nchini.
Bw.
Mkurya aliishauri Serikali kutumia mikusanyiko mbalimbali kutoa elimu
ya fedha ikiwemo nyumba za ibada na mikusanyiko mingine inayotambulika
na Serikali ili iweze kuwafikia wananchi wengi kwa mara moja.
Tags
HABARI ZA KITAIFA