Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 04
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 04 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA......!!! Polisi wakafika huko na kumkamata Saida na kuondoka na...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 04
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI

SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 04ILIPOISHIA......!!!
Polisi wakafika huko na kumkamata Saida na kuondoka naye huku wakimuacha Kareem akiwa na mawazo tele. Kilichokuja moyoni mwake, ilikuwa ni lazima kumuokoa Saida, hakutaka kuona msichana huyo akifa na wakati alikuwa akimpenda na tumboni alikuwa na mtoto wake.

SONGA NAYO
Saida aliwekwa ndani ya chumba cha sero huku akilia. Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama kweli safari yake ya kuelekea nchini Oman ingekuwa na mwisho namna hiyo.
Siku hiyo hakulala, mawazo yake yalikuwa juu ya wazazi wake, hakuamini kwamba mwisho wa kila kitu ungekuwa namna hiyo. Alijuta, aliumia moyoni mwake lakini hakuwa na jinsi kwani kwa kipindi hicho kilikuwa ni kusubiri kifo tu.
Taarifa za kukamatwa kwake, usiku huohuo zikaanza kusambazwa katika mitandao ya kijamii, hakukuwa na mtu aliyeamini mara baada ya kusoma taarifa ya msichana huyo na kuona kuwa ni Mtanzania.


Hapohapo taarifa zikaanza kusambaa kama moto wa kifuu mpaka zilipowafikia wazazi wake. Kwanza hawakuamini, hawakujua kilichokuwa kikiendelea nchini humo, wakaishia kulia tu kwani kwao, Saida alikuwa kila kitu hasa baada ya kumpa mwanaume wa Kiarabu, mtoto wa bilionea mkubwa katika nchi za Kiarabu.


Ndugu wakashtushwa, Dar es Salaam nzima stori ilikuwa kuhusu yeye. Hakukuwa na mtu aliyefurahia, kwa kipindi hicho, kila mtu akawa anailalamikia serikali ya Oman kwa kile ilichotaka kukifanya.


Wazazi na ndugu zake hawakulala, usiku mzima walikuwa wakiomboleza, kwao, Saida alikuwa kila kitu lakini kwa kipindi hicho alionekana kama mfu kwani hawakuwa na uhakika kama angenusurika, ilikuwa ni lazima auawe kama ilivyopangwa.


Kutokana na taarifa hizo kusambaa kwa kasi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ukanda wa Afrika Mashariki, bwana Omari Kidiru akawasiliana na balozi wa Oman nchini Tanzania na kuzungumza naye kuhusu jambo hilo.


“Nifanye nini sasa? Hizo ni sheria za nchi ambazo zilijiwekea tangu mwaka 1980, sina cha kufanya ila nitawasiliana nao wakuu nijue nini cha kufanya,” alisikika balozi wa Oman nchini Tanzania.


Siku iliyofuata, nchi nzima gumzo lilikuwa ni Saida. Picha zake akiwa amefungwa pingu zilisambaa kwa kasi kubwa katika mitandao ya kijamii. Kwa nchi za Kiarabu, ilikuwa ni lazima auawe siku hiyo kwani siku inayofuata ilikuwa ni siku ya Mfungo Mtukufu wa Ramadhan, kama wasingemhukumu siku hiyo, basi walitakiwa kusubiri mpaka mwezi uishe.


Kutokana na taarifa zile kusambazwa sana, mwisho wa siku zikafika katika Shirika la Haki za Binadamu. Shirika hilo likaingilia kati, halikutaka kuona mtu mwingine akiuawa kwa kupigwa mawe na wakati wao walikuwepo.


Wakaiambia serikali ya Oman kwamba hawakutakiwa kufanya kile walichotaka kukifanya lakini hawakueleweka hata kidogo, ilikuwa ni lazima kumuua Saida kwa sababu alivunja moja ya sheria za nchi hiyo.


“Ni lazima apigwe mawe mpaka kufa, haina jinsi, huwa hatuwezi kukaa na wazinzi,” alisikika Mwarabu mmoja aliyekuwa akisoma gazeti moja nchini humo.


Ilipofika saa nne asubuhi, Saida akachukuliwa na kupelekwa mahakamani. Kesi yake haikusikilizwa kwani uthibitisho wote wa kuonyesha kwamba alikuwa mjauzito ulipelekwa mahakamani hapo, kilichotolewa ni hukumu ya kupigwa mawe mpaka kufa katika Uwanja wa Kifo wa Al-Mederek uliokuwa pembezoni mwa Jiji la Muscat.


Hakimu akamtaka kushuka kizimbani, akachukuliwa na kupelekwa nje. Watu wote waliokuwa huko wakaanza kumzomea, waandishi wa habari waliokuwa hapo wakaanza kumpiga picha, stori yake ilikuwa kubwa na ndiyo ambayo ilisikika kila kona Oman.


Alilia lakini hakuna aliyemsikiliza, kila mtu alimzomea kwa kufanya kosa ambalo kwao lilionekana kuwa dhambi kubwa. Wengine wakatamani kumvamia na kumshambulia na kama kusingekuwa na ulinzi wa kutosha mahakamani hapo, Saida angeweza kupigwa vibaya na kufa hapohapo.


Ilikuwa ni aibu kubwa, watu wakamtaka avue baibui yake na kuvaa suruali, kwani kwa kitendo kile kilichotokea, hakutakiwa kuvaa nguo yoyote ya kuustili mwili wake. Akainama chini huku akilia, akachukuliwa na kupakizwa ndani ya gari dogo na kisha kuondolewa mahakamani hapo.


Walipofika sero, akashushwa na kisha kuandaliwa. Kitu cha kwanza kabisa, akaitiwa shehe na kuanza kuzungumza naye, ilibidi aanze kupewa mawahidha upya na ya mwisho, aombe msamaha na kusamehewa kwani dhambi aliyokuwa ameifanya, haikuwa ile isiyosameheka, ilitakiwa ajutie alichokifanya.


Hilo ndilo alilolifanya, akalia sana, alijuta mno, akaomba msamaha kwa kile alichokifanya kwamba shetani alimuingia na hakukusudia kufanya uasherati. Shehe alizungumza naye kwa dakika thelathini, akaondoka.


Saa saba baada ya swala, mlango wa sero ukafunguliwa na kisha kuchukuliwa na kuanza safari ya kuelekea katika Uwanja wa Uwanja wa Kifo wa Al-Mederek. Uwanja huo ulikuwa mkubwa na uliozungushwa kwa ukuta mkubwa. 


Kwa ndani, hakukuwa na kitu kingine zaidi ya mchanga na mashimo kadhaa huku kwa pembeni kukiwekwa mawe makubwa kwa ajili ya kumrushia mtu aliyehukumiwa kifo na kutakiwa kuuawa uwanjani hapo.


Hakukuwa na mtu aliyetakiwa kuingia ndani ya uwanja huo, watu wote walitakiwa kusimama nje kabisa wakati uwanja ukifungwa kwa ajili ya kusubiri watu wengine ambao walitakiwa kuuawa kwa sababu ya kupata ujauzito au kuhusika katika kulisaliti taifa lao kutoka kwa mataifa ya Magharibi.


Siku hiyo kulikuwa na idadi kubwa ya watu kwa kuwa kilipita kipindi kirefu hakukuwa na mtu aliyehukumiwa kifo cha aina hiyo. Watu walitamani kufanya mauaji ya aina hiyo na kutokana na wingi wa matangazo mitaani juu ya hukumu ya msichana Saida, ikawafanya watu wengi kukusanyika uwanjani hapo.


Saa moja baada ya hukumu kutolewa, tayari idadi kubwa ya watu wapatao elfu mbili walikwishafika nje ya geti la kuingilia ndani ya uwanja huo, kila mmoja alitaka kushiriki kumrushia mawe Saida. Nje, hakukukalika, kulikuwa na kelele na kila mtu alitaka kuona msichana huyo akifikishwa uwanjani hapo kwa ajili ya kuuawa.


Ilipofika saa saba na nusu, kwa mbali gari la polisi likaanza kuonekana barabarani likija mahali hapo. Kila mmoja alionekana kufurahia, watu wakajiandaa kwa ajili ya kumpokea msichana huyo, aingizwe ndani, afukiwe na kukiacha kichwa chake tu na watu waanze kumrushia mawe mpaka afe.


Baada ya gari hilo kufika hapo, watu wakatakiwa kukaa pembeni kwani msichana huyo angeteremshwa na kuingizwa katika uwanja huo na kuanza kurushiwa mawe. Watu wakatulia lakini Saida alipoteremshwa kutoka garini, wakaanza kumzomea.


Polisi wakamchukua mpaka getini ambapo mmoja akachukua ufunguo na kuingia ndani ya uwanja huo, watu wote wakaanza kuingia. Ndani hakukuwa na kitu zaidi ya mchanga na mashimo kadhaa.


Watu wote wakapigwa na butwaa, si wananchi tu bali hata polisi wenyewe. Kwa kawaida mawe hufikishwa humo siku moja kabla ya mtuhumiwa kuingizwa humo na polisi hufika na kufanya ukaguzi usiku kuhakikisha kwamba mawe yapo, cha kushangaza, hakukuwa na jiwe lolote lile.


Hali hiyo ikazua maswali mengi. Watu hawakuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Walichokifanya polisi ni kupiga simu katika kitengo cha waleta mawe ndani ya uwanja huo. Watu hao waliwaambia kwamba mawe ya kutosha yaliletwa uwanjani hapo usiku uliopita.


“Unasemaje?”
“Tulileta mawe jana usiku, majira ya saa moja,” alisikika mwanaume kwenye simu.
“Mbona hakuna mawe hapa.”
“Kweli?”
“Sasa nikudanganye ili iweje? Hakuna mawe. Leteni mawe kabla saa kumi,” alisema polisi huyo na kukata simu.


Huo ulikuwa uzembe mkubwa mno, hawakuamini kama kitu kile kingeweza kutokea. Waleta mawe walitakiwa kuyafikisha mawe hayo mahali hapo usiku uliopita, kwa kilichotokea, hakikuonekana kuwa cha kawaida hata kidogo.


Baada ya dakika kumi, wakapigiwa simu na kuambiwa kwamba gari la mawe lilikuwa njiani hivyo walitakiwa kusubiri. Hilo likawapa matumaini. Wakaendelea kusubiri zaidi na zaidi. 


Kutoka sehemu ya kuchukulia mawe mpaka hapo uwanjani hakukuwa mbali sana, ni ndani ya dakika kumi na tano tu, gari lilitakiwa kufika lakini kitu cha ajabu, mpaka dakika thelathini zinafika, gari halikuwa limefika.


“Mbona vijana wako hawajafika?” aliuliza polisi huku akionekana kukasirika.
“Hata mimi nimeshangaa sana. Kuna simu nilipigiwa na kuambiwa gari la kubeba mawe limepata ajali njiani baada ya dereva kumkwepa mtoto aliyekuwa akivuka barabara na gari kupinduka,” alisikika mwanaume huyo kwenye simu.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Yaani hapa sijui tufanye nini.”
“Tunabadilisha adhabu, tutamchapa kwa fimbo mpaka afe,” alisema polisi huyo.


Watu wakatangaziwa kile kilichokuwa kimetokea, kila mtu alihuzunika lakini baada ya kuambiwa kwamba adhabu ilibadilishwa, kila mmoja akaridhika. Ndani ya uwanja huohuo, mbali na mawe yaliyokuwa yakiwekwa, kulikuwa na fimbo, kama adhabu ya mawe ilishindikana basi mtu alitakiwa kuchapwa fimbo mpaka kifo chake.


Watu waliposikia kwamba adhabu ilibadilishwa na Saida alitakiwa kuchapwa fimbo zilizokuwa uwanjani hapo, kila mtu akakimbilia fimbo hizo na kuchukua zake zilizomtosha huku wengine wakiogopa kufanya hivyo.


Wanaume mia moja wakawa na fimbo zao mikononi, wakamuweka Saida katikati tayari kwa kumchapa fimbo kama ilivyokubaliwa. Wakati wakijiandaa kufanya kile kilichotakiwa huku Saida akiwa amefungwa kitambaa kichwa chake chote, mara wakaanza kusikia sauti ya mwanamke kutoka katika kundi lile la watu. 


Mwanamke huyo alikuwa akipiga kelele kwamba alikuwa na mabomu, hakuishia kupiga kelele tu bali akavua juba lake na kubaki na blauzi, watu walipomwangalia, walimuona akiwa na kikoti kilichokuwa na mabomu kadhaa.


Alipiga kelele kama kichaa, mbali na hilo, mkononi alishika kifaa kilichokuwa na kitufe ambacho kama angekiachia, mabomu yangelipuka, na mwenyewe alidai kwamba alichoka kukishika, kama kufa, ilikuwa bora akiachie na kufa na kundi hilo la watu.


Alikuwa akiomba msaada kwa kusema kwamba alitumwa kwa ajili ya kujitoa muhanga mahali hapo. Watu walipoyaona mabomu aliyokuwa amejivika, kwa jinsi watu walivyokuwa wakijitoa muhanga hapo Oman na nchi nyingine za Kiarabu, wote wakaanza kukimbia, si wananchi tu, hata polisi, kila aliyekuwa na fimbo, akaitupa na kuanza kukimbia kuyaokoa maisha yake.


“Bomu...bomu...bomu...” watu walipiga kelele, hata mlango wa kutokea ukaonekana mdogo, wengine wakaanza kuruka ukuta huo mkubwa ambao ulikuwa vigumu sana kuruka katika hali ya kawaida.


Kila mtu aliangalia maisha yake, kila mtu alitaka kuiokoa nafsi yake. Ndani ya sekunde ishrini tu, ndani ya uwanja huo walibaki watu wawili tu. Saida na mwanamke huyo aliyekuwa na mabomu ambaye muda wowote ule alikuwa akilia kuomba msaada.


Je nini kitaendelea? Tukutane Saa Moja Usiku mahali hapa.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top