SERIKALI INATAMBUA UMUHIMU WA KUKUZA USAWA WA KIJINSIA – MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kama njia mojawapo ya kuimarisha ustawi na kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.

Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha jamii ya Watanzania inaishi kwa umoja na mshikamano kati ya wanaume na wanawake na kuwa wote wanapata huduma za msingi kwa haki na usawa katika nyanja zote ikiwemo kisheria, elimu, afya, uchumi na nafasi za maamuzi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Alhamisi, Machi 6, 2025 alipozungumza na wananchi katika Kongamano la Wanawake Kanda ya Kusini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika Kitaifa Machi 8, jijini Arusha. Kongamano hilo limefanyika katika viwanja vya Maegesho, Nachingwea mkoani Lindi.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi Serikali imeendelea kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri na kutoa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mikopo hiyo imewawezesha wanawake kutekeleza miradi kwa lengo la kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na pato la Taifa kwa ujumla.

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuiagiza mikoa yote nchini iandae mkakati na mpangokazi wa utekelezaji maazimio ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa mwaka 2025 ili uwe msingi wa tathmini baada ya miaka mitano ya utekelezaji.

“Wanawake endeleeni kuhamasishana kutumia fursa za uwepo wa madirisha yenye huduma za mikopo kwa wanawake kujikwamua kiuchumi. Nendeni kwenye benki zinazotoa huduma hizo zilizoko karibu nanyi mpate mikopo hiyo inayotolewa kwa masharti nafuu na hakikisheni mnarejesha kwa wakati mikopo yote mnayopata, ili wananchi wengine waweze kukopa.”

Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Amon Mpanju alisema Wanawake ni muhimili na chachu kubwa ya kuleta maendeleo katika ngazi ya familia na Taifa kwa ujumla, hivyo kongamano hilo linalenga kuweka mikakati ya kuendelea kumkwamua mwanamke kiuchumi.

Pia, Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa rai kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

"Wakati ukifika wanawake jitokezeni kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ili mshiriki katika kutoa maamuzi".

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post