GSM Foundation kwa kushirikiana na Hospitali ya CCBRT na klabu ya Yanga waliendesha Harambee ya Mwezeshe atembee kwa ajili ya kukusanya fedha ili kutibu watoto 400 wenye Mguu Kifundo 'ClubFoot' katika Hospitali bingwa ya CCBRT.
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dr. Emmanuel Nchimbi aliambatana na Mufti mkuu wa Bakwata, Dr. Abubakar Bin Zubeir waliungana na Ghalib Said Mohamed ambaye Taasisi yake ndio iliyoandaa tukio hilo kubwa.
Zaidi ya Tsh bilioni 1 zilikusanywa na kuvuka malengo ya kukusanya Tsh 600M fedha ambazo ndizo zilizohitajika kwa ajili ya matibabu ya watoto hao.
Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema fedha hizo zitakwenda kuhudumia watoto wenye Mguu Kifundo ambapo takribani watoto 2,000 huzaliwa kila mwaka nchini Tanzania wakiwa na taatizo hilo.
"Watoto hawa wakipata matibabu wataepuka kilema cha milele na wakikosa matibabu ni kinyume chake, ulemavu wa milele. Shujaa wetu Dr. Brenda Msangi, CEO wa Comprehensive Community Based Rehabilitation Tanzania (CCBRT) ataendesha jahazi hili la MWEZESHA ATEMBEE," alisema Hersi.
Katika Harambee hiyo GSM alichangia Tsh Milioni 100 huku picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ikiuzzwa Tsh Milioni 104.
Picha hiyo ilinunuliwa na Wizara ya Afya, Benki ya NMB, Benki ya CRDB pamoja na Katibu wa CCM Dkt. Emanuel Nchimbi.
Tags
HABARI ZA KITAIFA