Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, chini ya uongozi wa Makamu Mwenyekiti wake, Mhe. Rajab Msaka, limekubali na kupitisha mapendekezo ya kugawa Majimbo ya Uchaguzi ya Kilwa Kusini na Kilwa Kaskazini kwa lengo la kuanzisha Jimbo Jipya la Kilwa Mashariki.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, majimbo matatu yatakuwa na mipaka ifuatayo: Jimbo la Kilwa Kaskazini litakuwa na Kata ya Kipatimu, Kandawale, Chumo, Namayuni, Kibata, Mingumbi, Kinjumbi, na Somanga.
Jimbo la Kilwa Kusini litakuwa na Kata ya Pande, Lihimalyao, Mandawa, Kiranjeranje, Nanjirinji, Likawage, Njinjo na Miguruwe.
Jimbo la Kilwa Mashariki litakuwa na Kata ya Songosongo, Masoko, Kivinje, Tingi, Miteja, Kikole na Mitole.
Sifa za majimbo hayo ni kama ifuatavyo: Jimbo la Kilwa Kaskazini litakuwa na idadi ya watu 94,845 na eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,074.63.
Jimbo la Kilwa Kusini litakuwa na idadi ya watu 112,682 na eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 8,959.68. Jimbo la Kilwa Mashariki litakuwa na idadi ya watu 90,149 na eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,313.18.
Takwimu hizi zinatokana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2022.
Vilevile, ni muhimu kutambua kuwa ugawaji wa majimbo hayo umezingatia vigezo vyote vilivyopendekezwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.