Yanga imeendeleza ubabe wake kileleni mwa msimamo wa Ligi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo wa kusisimua uliofanyika uwanja wa CCM Kirumba.
Pamba Jiji walionesha ari ya mapema kwa kushambulia lango la Yanga, lakini ni Wananchi waliokuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika ya 28 kupitia kwa Chadrack Boka, aliyejaza mpira wa faulo kutoka nje kidogo ya 18.
Katika mchezo huo, kocha Miloud Hamdi alionyesha mbinu za kipekee kwa kuanzisha viungo watatu wa ulinzi – Khalid Aucho, Mudathir Yahya, na Duke Abuya – ili kupambana na presha iliyozidi kutoka kwa Pamba Jiji.
Kipindi cha pili kilionyesha mabadiliko ya kimikakati, ambapo Miloud alimuingiza Stephane Aziz Ki kuchukua nafasi ya Aucho. Mabadiliko haya yaliifanya Yanga kuwa na kasi zaidi ya mashambulizi.
Aziz Ki alijitokeza kuwa shujaa wa Yanga katika kipindi cha pili, akiifungia timu yake mabao mawili muhimu yaliyoihakikishia ushindi. Bao la pili alilifunga kwa mpira wa krosi aliopokea kutoka kwa Jonathan Ikangalombo, ambaye alichukua nafasi ya Mudathir Yahya kwa mara ya kwanza msimu huu.
Ikangalombo alionyesha umahiri wake kwa kuhusika moja kwa moja kwenye upatikanaji wa bao la pili. Alitoa pasi kwa Maxi Nzengeli, ambaye alikata krosi kwa Aziz Ki. Pamoja na umahiri wa Ikangalombo, nafasi nyingine nzuri alizozitengeneza kwa Aziz Ki zilishindwa kutumika.
Kwa ushindi huu, Yanga inapata alama tatu muhimu na kufikisha jumla ya alama 58 baada ya mechi 22, huku wakijiandaa kwa mchezo wa Kariakoo Derby dhidi ya Simba, utakaochezwa Machi 8.