Bondia wa ngumi za kulipwa kutoka Tanzania, Kennedy Ayo amepima uzito kwaajili ya pambano lake la raundi 10 litakalofanyika kwenye ukumbi klabu ya mchezo wa ngumi wa Brown uliopo katika eneo la Kulambiro jijini Kampala nchini Uganda.Ayo amekamilisha zoezi hilo la kupima uzito pamoja na mpinzani wake Henry Kigongo wa nchini Uganda kuelekea pambano lake hilo la uzani wa 'welter' la kimataifa litakalo fanyika Februari 28, 2025.
Ayo anaenda kucheza pambano lake la pili la kimataifa baada ya lile la mwisho aliloshinda nchini Urusi dhidi ya mpinzani wake Ismat Guliyev lililofanyika Disemba 13, 2024.
Ayo ni bondia namba sita nchini Tanzania kati ya mabondia 53 na Duniani ni wa 286 kati ya 1973 akiwa na nyota moja na nusu katika uzani wa 'middle' huku akicheza mapambano nane akishinda sita kati ya hayo ameshinda mawili kwa 'KO' na kupoteza mawili ambayo yote amepigwa kwa 'KO'
Ayo atapanda ulingoni kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika mashariki.
Naye Kigongo ambaye ni mpinzani wa Ayo ni bondia namba 2 nchini Uganda kati ya mabondia 28 na Duniani ni wa 113 kati ya 2458 akiwa na nyota mbili na nusu katika uzani wa 'welter'.
Mbali na Ayo pia Mtanzania mwengine atakayepigana kesho ni Salum Gumbo atakayepigana na bondia wa Uganda Joshua Tusingwire. Gumbo atapanda ulingoni kuanzia saa 9:00 alasiri kwa saa za Afrika mashariki.
Pambano hilo litaoneshwa mubashara kupitia kituo cha Nara Boxing tv cha nchini Uganda kupitia Youtube.
"Watanzania watarajie mchezo mzuri kwasababu Kennedy Ayo na Salum Gumbo ni mabondia wazuri na wapinzani wao ni wazuri pia," amesema Feisal Ashinda ambaye aliyewatafutia pambano hilo mabondia hao wa Tanzania.
Tags
HABARI ZA KITAIFA